TFDA yakamata bidhaa zilizokwisha muda wake

09Feb 2016
Morogoro
Nipashe
TFDA yakamata bidhaa zilizokwisha muda wake

MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA), Kanda ya kati, imekamata shehena ya bidhaa zilizokuwa zimehifadhiwa na mfanyabiashara kinyume na taratibu katika kata ya Kihonda, Manispaa ya Morogoro.

Baadhi ya bidhaa hizo zilikuwa zimehifadhiwa chooni hali inayohatarisha afya za watumiaji.

Katika eneo la Kihonda, maofisa wa TFDA walifanikiwa kuingia kwa mfanyabiashara mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Shabani na kukuta bidhaa mbalimbaki zikiwa zimehifadhiwa kinyume na utaratibu.

Mkaguzi wa Chakula na Dawa kutoka TFDA Kanda ya Kati Dk. Engerbet Mbekenga, alisema awali mfanyaniashara huyo aliwahi kukamatwa na wakaguzi wa Mamlaka hiyo na kulipishwa faini ya Sh. 600,000 baada ya kukutwa amehifadhi vinywaji maeneo ya chooni, sambamba na bidhaa nyingine zilizokwisha muda wa matumizi, hali iliyokua ikihatarisha afya za watumiaji wa bidhaa hizo anazozihifadhi na kuziuza kibiashara.

Hata hivyo, mtuhumiwa huyo pamoja na kuthibitisha angekwenda kuzitekeza mwenyewe bidhaa hizo hakufanya hivyo na TFDA walitilia shaka na kufanya ukaguzi mwingine wa kushtukiza na kubaini hali ikiwa inaendelea kama ilivyokuwa awali kabla ya onyo na faini.

Awali baada ya maofisa wa TFDA kufika dukani kwa mfanyabiashara huyo, aligoma kufungua geti kwa madai kuwa yeye siyo mhusika na kuanza kuhamisha bidhaa hizo hivyo kuwalazimu maofisa hao kuingia kwa nguvu ndani.

Baada ya ukaguzi, maofisa wa mamlaka hiyo waligundua udanganyifu unaofanywa na mfanyabiashara huyo kwani hakuwa ameteketeza bidhaa alizokua ameagizwa kufanya hivyo na badala yake aliamua kuendelea kuziuza kwa wateja wake.

Dk. Mbekenga alimuagiza mfanyabiashara huyo kulifunga duka hilo na kusitisha shughuli zote za kibiashara hadi pale sakata hilo litakapofikishwa mahakamani ikiwemo kwa makosa ya kukaidi amri halali ya mamlaka hiyo na kuendelea kufanya biashara kinyume na taratibu.

TFDA na Ofisa Afya wa Manispaa ya Morogoro, Beatrice Nambisa walichukua baadhi ya bidhaa na kwenda kuziteketeza, huku waliahidi kubuni mbinu zaidi kupambana na watuhumiwa wa aina hiyo.

Habari Kubwa