Thamani ya uwekezaji EPZ yafikia bil. 144/-

23Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Thamani ya uwekezaji EPZ yafikia bil. 144/-

UWEKEZAJI wa kampuni 11 zilizosajiliwa na Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA), kuwekeza katika viwanda vilivyoko kwenye maeneo maalum ya uwekezaji (SEZ) wilayani Bagamoyo, umeongezeka na kufikia Dola milioni 62.84 ( takribani Sh. bilioni 144.53).

Aidha, mapato ya fedha za kigeni yanayotarajiwa kupatikana kutokana na mauzo ya bidhaa za kampuni hizo nje ya nchi ni takribani Dola milioni 76.96 (karibu Sh. bilioni 177) wakati huohuo, zikizalishwa zaidi ya ajira 1,614.

Mkurugenzi wa Uwezeshaji Uwekezaj wa EPZA, James Maziku, alisema haya mjini Kibaha, mkoani Pwani katika maonyesho ya viwanda na uwekezaji yanayoendelea mkoani hapa.

Alisema uwekezaji na ujenzi wa viwanda vya kampuni mbili zilizosajiliwa katika maeneo maalumu ya uwekezaji wilayani Bagamoyo, umekamilika na kuanza kazi na nyingine zimefikia katika hatua mbalimbali.

Kampuni mbili ambazo zimekamililsha ujenzi wa viwanda ni Africa Dragon Enterprises Ltd, ambacho kilianza kazi mwaka 2017 kikijihusisha na uzalishaji wa nyaya zilizopakwa madini ya chuma.

Kiwanda kingine ni Phiss Tannery Limited kinachozalisha wa ngozi na bidhaa zake tangu mwaka 2013.

Pamoja na mafanikio hayo makubwa, alisema kampuni hizi zinakutana na vikwazo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa miundombinu ya viwanda na usafiri na ugumu wa kuuza katika soko la ndani na la Afrika Mashariki.

Maziku alisema uwekezaji katika maeneo maalum ya uwekezaji wa Bagamoyo upo katika hatua za mwanzo kabisa huku ukikumbwa na changamoto kama kukosekana kwa umeme, maji, usambazaji wa gesi katika eneo lote la mradi.

“Serikali ndiyo yenye jukumu la kuweka miundombinu hii katika maeneo maalum ya uwekezaji ya Bagamoyo ili kuongeza ufanisi na kuvutia uwekezaji zaidi. Kutokana na hii, wawekezaji wanaingia gharama zaidi ya kujenga miundombinu wezeshi,” alisema Maziku.

Changamoto nyingine ni ubovu wa barabara katika eneo hili la uwekezaji ambao umekuwa ukikwamisha usafiri wa shehena kama malighafi kwa ajili ya viwanda na bidhaa kupelekwa sokoni.

Pia kampuni hizo zimekuwa zikikumbana na ugumu wa kuuza bidhaa zao katika soko la ndani na la Afrika Mashariki kutokana na kodi kubwa inayotozwa katika bidhaa wanazozalisha.

Kwa mfano, bidhaa zinazozalishwa kwenye maeneo maalum ya kiuchumi zinatozwa asilimia 23 ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ukilinganisha na asilimia 18 inayotozwa biashara ya kawaida nchini.

Habari Kubwa