TIC yasajili miradi ya uwekezaji 87 ya bil. 40/-

12Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
ARUSHA
Nipashe
TIC yasajili miradi ya uwekezaji 87 ya bil. 40/-

KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kimesema kwamba kilisajili miradi ipatayo 87 ya uwekezaji yenye thamani ya dola za Marekani milioni 1,482.23 (sawa na Sh. bilioni 40) kati ya Julai na Desemba mwaka 2018.

KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Miradi hyo ilitarajia kutoa ajira mpya kwa zaidi ya Watanzania 11,191 katika sekta  mbalimbali.

Aliyebainisha hayo ni Meneja wa TIC Kanda ya Kaskazini, Daud Riganda, wakati wa maonyesho ya pili ya Karibu Kili-Fair yaliyomalizika jijini Arusha hivi karibuni.

Kati ya miradi 87 iliyosajiliwa ama kuandikishwa na TIC kwa upande wa  sekta ya utalii hususan ujenzi wa mahoteli na kampuni za uwakala wa utalii, Riganda alisema kuwa kituo hicho kilisajili miradi takribani kumi.

Alitaja miradi ya mingine ni minne katika sekta ya kilimo, majengo ya biashara ni miradi 11 na miradi ya nishati iliandikishwa  miwili.

Alisema mbali na miradi hiyo, TIC pia ilisajili na kuandikisha mradi mmoja wa taasisi ya fedha, shule na afya.

Aidha, Riganda alisema kwamba kulikuwa na miradi ya huduma ipatayo saba, utangazaji mradi mmoja, masuala ya maliasili mmoja na miradi  ya usafirishaji takribani saba.

Riganda alieleza kwamba kati ya miradi yote hiyo 87 iliyosajiliwa na kituo hicho nchini katika kipindi hicho, miradi 52 sawa na asilimia 60 inamilikiwa na Watanzania.

Kwa mujibu wa Riganda, miradi 33 sawa na asilimia 38 inamilikiwa na wageni na  asilimia mbili ambapo ni mradi mmoja unaendeshwa  kwa ubia kati ya Watanzania na wageni.

Alieleza kwamba kutokana na takwimu hizi,  inaonyesha kwamba hivi sasa  Watanzania wameamka na wameanza kuchangamikia fursa za uwekezaji.

Alizitaja nchi nyingine nne zinazoongoza kwa uwekezaji nchini kuwa ni China,  Uingereza, Marekani na India.

Aidha, kwa upande wa nchi za Afrika  zinazoongoza kwa uwekezaji nchini Mauritius, Afrika Kusini na Kenya.

Akifafanua kuhusiana na kituo hicho kinavyorahisisha mazingira ya uwekezaji nchini, Riganda alieleza kuwa katika kipindi hicho walishughulikia maombi ya huduma za ukaazi daraja la A za uwekezaji 258 na   maombi ya daraja B 1,119.

Alisema kwamba katika kipindi hicho TIC ilitoa vibali vya kufanya kazi nchini takribani 1,248.

Alisema TIC ilishughulikia maombi yanayohusu masuala ya kodi kwa wawekezaji takribani 146 na kutoa leseni za biashara 40 katika kipindi hicho cha miezi sita.

Meneja huyo wa TIC Kanda ya Kaskazini, alieleza kwamba katika masuala yanayohusu mazingira, TIC walishughulikia na kusajili maombi 11 na maombi ya masuala ya ardhi kwa wawekezaji 248.

Habari Kubwa