Ticts yajivunia ongezeko la huduma

26Jan 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Ticts yajivunia ongezeko la huduma

KAMPUNI ya Kimataifa ya Huduma za Makontena Bandarini (Ticts), imehudumia shehena 592,000 kwa kipindi cha mwaka jana.
 

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Ticts, Jared Zerbe, aliyabainisha hayo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya kampuni katika kipindi cha mwaka jana ikilinganishwa na miaka iliyopita.
 
Alisema Agosti, mwaka jana, walihudumia makontena 54,447 na kuweka rekodi ya makontena 31,239 yanayohudumiwa katika geti kwa mwezi wa Machi.
 
“Ongezeko la shehena ya ndani kwa ajili ya nje ya nchi limefikia asilimia 18, zaidi ya mwaka 2017. Mizigo ambayo inatoka nchi mbalimbali zikiwamo Congo na Zambia wanaotumia bandari yetu, iliongezeka kwa wastani asilimia 38.9 kwa mwaka 2018,"alisema Zerbe.
 
Alisema ongezeko la shehena linahitaji ufanisi na uharaka katika utoaji mizigo ili kupunguza muda wa mizigo kukaa bandarini, hivyo kampuni hiyo na bandari zimeongeza ufanisi na uwezo wa kuhudumia shehena kubwa zaidi.
 
“Msaada wa ushirikiano tunaopata kutoka kwa serikali ya Tanzania, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato (TRA), wafanyakazi, wateja na wadau wanaotumia bandari hii, kimekuwa chanzo cha ukuaji wa huduma za Ticts katika mwaka 2018.

“Binafsi najivunia kwa timu yetu nzuri sana ya wafanyakazi wa Ticts ambao wamekuwa wakifanya kazi pamoja vizuri na kupambana na ongezeko la kuhudumia shehena,” alisema Zebre.
 
Naye Mkurugenzi wa Huduma wa Ticts, Donald Talawa, alisema kutokana na juhudi walizoongeza kwenye kampuni hiyo, wamejipanga kuhudumia ongezeko la mizigo.
 
“Tunaongeza ufanisi ili kuhudumia shehena hii inayokuwa, Ticts imejikita kusonga mbele na kuimarisha wajibu wake kama lango kuu la nchi kuelekea Mashariki, Kusini na Afrika ya Kati,” alisema Talawa.