TMDA kudhibiti uingizaji bidhaa zisizosajiliwa

06Aug 2020
Grace Mwakalinga
Mbeya
Nipashe
TMDA kudhibiti uingizaji bidhaa zisizosajiliwa

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), imeahidi kufanya msako wa kudhibiti na kuzuia uingizwaji pamoja na uuzaji wa bidhaa zisizosajiliwa na mamlaka hiyo na kuweka ulinzi kwenye njia za panya katika mikoa ya Songwe, Rukwa na Mbeya.

Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TDMA), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Anitha Mshighati, akionyesha sampuli za dawa na vifaa tiba, ambavyo vinaruhusiwa na mamlaka hiyo, kutumika katika maonyesho ya wakulima Nanenane katika viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya, jana. PICHA: GRACE MWAKALINGA

Kauli hiyo ilitolewa jana na Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Nyanda za Juu kusini, Anita Mshighati, wakati akizungumza na Nipashe, kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia uuzaji wa bidhaa ambazo hazijathibitishwa na mamlaka yao ni uwapo wa njia za panya kwenye mikoa hiyo ambayo wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu hupitisha vifaa tiba na dawa.

Alisema baada ya kubaini uingizwaji holela wa dawa na vifaa tiba, mamlaka hiyo imeanzisha operesheni ya kukagua na kuangalia bidhaa zinazopitishwa kwenye mipaka pamoja na kudhibiti njia za panya kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya.

“Nchi yetu ni kubwa kuna mipaka ambayo siyo rasmi watu wasio waaminifu hutumia njia hizo kupitisha bidhaa ambazo hazina ubora wowote, maeneo kama Songwe na Rukwa, inapatikana na nchi jirani hivyo mwingiliano ni mkubwa bidhaa nyingi zinauzwa huko hivyo katika kudhibiti hilo tumekuwa tukishirikiana na halmashauri,” alisema Mshighati.

Alisema moja ya majukumu ya mamlaka hiyo ni kutoa vibali vya kuingiza na kutoa bidhaa ambazo ni dawa, vifaa tiba na vitendanishi ambazo zimethibitishwa na mamlaka zote ikiwamo ya TMDA.

Pia alisema bado wananchi hawana taarifa ya kutosha kuhusu mamlaka hiyo kuhama kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na kuwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), kwa kuwa bado wanaendelea kutoa taarifa za masuala ya vyakula vinavyotiliwa shaka.

Aliwahamasisha kutumia dawa kulingana na maelekezo ya wataalamu wanayopewa ili wasiweze kupata madhara kwa kuhakikisha wanaangalia muda wa matumizi kuisha kabla ya kutumia.

Aliwakumbusha wananchi kutoa taarifa wanapobaini uingizwaji holela wa dawa pamoja na taarifa kwa yeyote anayepata madhara baada ya kutumia dawa.

Mkazi wa Kigoe wilayani Mbarali, Bahati John, alisema maonyesho ya Nanenane yamempa fursa ya kujifunza masuala mbalimbali ikiwamo elimu juu ya dawa na vifaa tiba, huku akisema kikubwa ni kukagua na kuangalia muda wa matumizi ya dawa hizo.

Habari Kubwa