TMDA yatoa vibali 26,478 kimtandao

05Dec 2019
Devota Mwachang'a
Dodoma
Nipashe
TMDA yatoa vibali 26,478 kimtandao

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), imetoa vibali 26,478 katika mwaka 2018¬/19 sawa na ongezeko la asilimia 203 ukilinganisha na 13,018 mwaka 2015/16 kwa njia ya mfumo wa kieletroniki wa utoaji wa vibali.

Mfumo huo unamwezesha mteja kutuma maombi, kufanya malipo popote alipo kisha kupata kibali ndani ya saa 24.

Katika taarifa ya kiutendaji ya mamlaka hiyo iliyotolewa na kusainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo, amesema wameongeza udhibiti wa uingizaji na usafirishaji wa bidhaa ndani na nje ya nchi kupitia mfumo wa kieletroniki wa utoaji vibali.

Fimbo alisema utoaji huduma za vibali kwa wateja umerahisishwa kwa kiasi kikubwa kupitia mfumo wa IMIS ambao umetumika kuweka taarifa na takwimu za TMDA zikiwamo za bidhaa, majengo yaliyosajiliwa na za wateja, na kuwa wanaweza kuleta maombi yao kwa mtandao bila kufika ofisi za TMDA.

“Kwa lengo la kutekeleza agizo la Rais John Magufuli, la Mei, 2017 linalolenga kuharakisha utoaji wa mizigo bandarini, Mamlaka imeweka wakaguzi wake ambao hufanya kazi saa 24 kwa siku zote za juma, na kufanikiwa kufikia na kuvuka malengo iliyojiwekea katika udhibiti wa ubora, usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi ili kulinda afya ya jamii,” alilezea Fimbo.

Aidha, alisema: “Kwa miaka minne ndani ya uongozi wa Rais Magufuli tumefanikiwa kutekeleza mpango wa ufuatiliaji wa ubora wa bidhaa katika soko, sampuli 1,136 za dawa za binadamu zilifuatiliwa na kuchunguzwa katika kipindi hiki ambapo asilimia 96 ziliendelea kukidhi vigezo vya ubora.

Kwa mujibu wa fimbo, TMDA imeanzisha mfumo wa kielektroniki wa ufuatiliaji utoaji wa taarifa za madhara yatokanayo na matumizi ya dawa na vifaa tiba kwa kutumia simu za mkononi au kompyuta na njia ya kutuma ujumbe wa simu.

Ameeleza kuwa Mamlaka imefanikisha uchunguzi katika mwaka 2017/18, jumla ya tani 140,705.25 za bidhaa dawa, na vifaa tiba zisizofaa kwa matumizi ya binadamu zenye thamani ya takribani Sh. 22,394,078,744 ziliteketezwa ikilinganishwa na tani 664.68 zilizoteketezwa mwaka 2018/19.

Pia amesema TMDA imeimarisha shughuli za maabara kwa kuongeza vifaa vya uchunguzi pamoja na ufungaji wa maabara ndogo 25 zinazohamishika katika vituo vya forodha kwaajili ya uchunguzi wa awali wa bidhaa.

Matokeo ya uchunguzi wa sampuli yanaonesha kuwa bidhaa zilizochunguzwa zimekidhi viwango vya ubora na usalama kwa wastani wa asilimia 90.

Fimbo amesema kwa tathmini iliyofanywa usajili wa bidhaa za dawa, vifaa tiba na vitendanishi umeendelea kuimarika ambapo idadi ya bidhaa zilizosajiliwa imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka, katika kipindi cha miaka 2015/16 hadi 2018/19, jumla ya bidhaa 20,247 zimesajiliwa.

Hii imetokana na kuongezeka kwa uelewa wa matakwa ya sheria miongoni mwa wafanyabiashara na kukua kwa biashara.

Fimbo alisema mamlaka imesimamia vyanzo vya makusanyo kwa ajili ya udhibiti ambapo bajeti imeongezeka kutoka Sh. bilioni 34.64 mwaka 2015/16 hadi Sh. bilioni 53.31 mwaka 2018/19 sawa na asilimia 53.8. Hii imewezesha utoaji huduma kwa ufanisi na kutoa gawio kwa Serikali kila mwaka hadi kufikia takribani Sh. bilioni 29.

Habari Kubwa