TPA yatenga mil. 50/- kusaidia maendeleo

19Mar 2019
Dege Masoli
Tanga
Nipashe
TPA yatenga mil. 50/- kusaidia maendeleo

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imetenga Sh. milioni 50 kwa Mkoa wa Tanga kuchangia shughuli za kijamii
katika miji inayozunguka bandari ikiwa ni mpango wa bajeti ya mwaka 2018/2019.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deodatus Kakoko, alisema fedha hizo ni mpango wa kuchangia kupitia asilimia za mapato yake utakaotolewa katika maeneo muhimu ya kijamii kama elimu na afya.

Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi mabati 379 ya Shule ya Ufundi ya Tanga iliyofanyika mwishoni mwa wiki shuleni hapo, Kakoko
alisema pamoja na bati hizo, Mamlaka hiyo itachangia huduma za afya Wilaya ya Pangani.

Alisema uchangiaji huo ni utekelezaji wa sera ya Bodi ya Mamlaka hiyo na pia jamii inayoishi katika maeneo hususani yaliyozungukwa na Bandari na nchi nzima itanufaika na mpango huo.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TPA, Ignas Rubaratuka, alisema lengo la uchangiaji huo ni kuboresha mazingira ya shule hiyo pamoja na makazi ya walimu ili kuinua kiwango cha elimu.

Awali Mkuu wa shule hiyo, Andrew Mwakanyamale, alieleza changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni uchakavu wa nyumba za walimu, majengo ya shule, kantini, shule ya awali na kutokuwa na uzio jambo linalohatarisha usalama wa wanafunzi na mali za shule.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa, alipongeza mpango wa mamlaka hiyo kusaidia shughuli za kijamii na kwamba Tanga umewafikia wakati mwafaka.

Mwilapwa alieleza umuhimu wa mpango wa mamlaka hiyo kuwa uchangiaji huo utarahisisha pia utekelezaji wa sera ya elimu bure na hivyo kufikia lengo la kila mtoto kusoma.