TPB, TADB, NMB kusaidia wakulima wadogo

17Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
TPB, TADB, NMB kusaidia wakulima wadogo

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeingia makubaliano na Benki za Biashara za NMB na Benki ya Posta (TPB) lengo kuwasaidia wakulima wadogo wadogo kupitia Mfuko wa Dhamana kwa Wakulima Wadogo chini ya TADB.

Makubaliano hayo yalifikiwa ili kumwezesha na kumwinua mkulima mdogo aweze kumudu kilimo chenye tija, kupunguza umaskini na kufikia malengo ya serikali ya kufikia uchumi wa kati na viwanda ifikapo 2025.

Akizungumza baada ya kikao cha pamoja cha wakuu wa mikopo wa benki hizo tatu pamoja Meneja anayesimamia mfuko huo Jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa Mfuko huo, James Mwakilima, alisema serikali imeshatoa Shilingi bilioni 45 kwa mfuko kwa ajili ya kuwakopesha wakulima wadogo sehemu mbalimbali nchini.

“Katika kutimiza azma yake ya kujenga uchumi wa kati na viwanda, serikali imeshatoa Shilingi bilioni 45 kwa TADB kupitia mfuko wake wa dhamana kwa wakulima wadogo, ili wakulima waweze kujikita kwenye kilimo chenye tija.” Alisema Mwakilima.

Alitoa wito kwa wakulima nchini kuitumia vyema fursa hiyo, kwa kuwa itakuwa fahari kubwa kwa Benki ya Kilimo kuona wakulima wanainuka kiuchumi na kufikia malengo ya serikali ya uchumi wa kati na viwanda, kwa kuwa hakuna viwanda visivyo na malighafi.

“Ni nafasi pekee kwa wakulima wadogo hapa nchini kuitumia vyema fursa hii kwa kuwa Benki ya Kilimo ni moja ya madaraja ya kumvusha mkulima kutimiza malengo yake,” alisisitiza Mwakilima.

Kaimu Mkurugenzi wa Mikopo wa TPB, Ramadhan Mganga, alisema kupitia Mfuko huo benki yake imefanikiwa kuwakopesha wakulima wadogo nchini.

“Kupitia mfuko huu wa dhamana kwa wakulima wadogo, Benki ya Posta imewakopesha wakulima zaidi ya Shilingi bilioni 3.5 kwa kipindi cha miezi sita tu tangu tusaini makubaliano,” alisema Mganga.

Alitaja mikoa ambayo imenufaika na mikopo ni Simiyu, Iringa na Singida ambapo Shilingi bilioni 3.5 zilikopeshwa.

“Zaidi ya bilioni 3 zimekopeshwa kwa wakulima katika mikoa ya Morogoro, Iringa na Singida, huku tukiendelea kufanya utafiti katika mikoa mbalimbali ili tuweze kumsaidia mkulima kuinua kipato chake,” alisema.

Katika kuhakikisha wakulima wananufaika na mikopo hiyo, Benki ya Posta imekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu kwa wakulima wadogo juu ya mazao gani walime na kwa wakati gani, ili waweze kuwa na kilimo chenye tija.

“Licha ya kutoa mikopo kupitia matawi yetu yaliyopo nchi nzima, lakini pia tumekuwa na nafasi ya kutoa elimu juu ya mikopo, mazao yanayotakiwa kulimwa na wakati gani yalimwe ili yasimpe mkulima hasara,” alisema Mganga.

Habari Kubwa