TPRI yatia mguu vita gugu karoti

09Feb 2018
Allan lsack
ARUSHA
Nipashe
TPRI yatia mguu vita gugu karoti

TAASISI ya Utafiti wa Viuatilifu vya kudhibiti visumbufu katika Ukanda wa Tropiki (TPRI) imepata njia mbadala ya kibaolojia itakayosaidia kuteketeza majani ya gugu karoti na vijidudu vinavyoshambulia mazao mashambani.

gugu karoti.

Akizungumza katika semina ya utoaji wa elimu kuhusu madhara ya gugu karoti katika Halmashauri ya Arusha Vijijini juzi, mtafiti kutoka TPRI, Ramadhani Kilewa, alisema lengo la semina hiyo ni kuwajengea wananchi uwezo wa kutambua madhara yanayotokana na majani hayo.

Alisema wamepokea madudu kutoka Afrika kusini ambayo yatakula majani hayo hadi yatapokausha katika eneo husika na wakati huo yakindelea kuzaliana na kusambaa kwa upepo au maji kwenye maeneo mengine.

“Lengo letu ni kutatua matatizo yanayowakabili wakulima vijijini kama iliyokuwa dhamira ya serikali kuhakisha kero zinazowakabili wakulima zinatafutiwa njia mbadala ili kuwasaidia kuzalisha mazao ya kutosha ambayo yatatupunguza wimbi la umaskini kwa wananchi vijijini,” alisema.

Akizungumzia madhara ya kiafya yatokanayo na mmea huo, Kilewa alisema pindi watu wanaposhika bila kuwa na vitendea kazi itawasababishia kupata ugonjwa wa ngozi.

Aidha alisema kutokana na vumbi linalotokana kwenye mmea huo, husababisha watu kupata maradhi ya pumu.Kwa upande wa sekta ya kilimo mmea huo umesababisha madhara kwa ardhi kupoteza rutuba, kupoteza uzalishaji wa mazao kwa asilimia 80 kwa sababu linastawi kwa haraka na kuchukua sehemu kubwa ya ardhi.

Akizungumzia njia ya kulidhibiti, Kilewa alisema watu wanapaswa kuling’oa na kuchoma wakati huo wakiwa wamevaa nguo zinazofunika mwili mzima ambazo zitasaidia kuzuia moshi usiingie mwilini na kuleta madhara ya ngozi.

Sambamba na hilo njia nyingine alizotaka wananchi kuzitumia ni pamoja na kuweka wadudu na kutumia kemikali.

Kaimu Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Margaret Mollel, alieleza kuwa tofauti na binadamu pia gugu karoti limeleta madhara kwa wanyama kufa wanapokula majani hayo.

“Mnyama anapokula majani hayo, kwa kiasi cha asilimia 30 hadi 50 anakufa, halafu utakapokwenda kuangalia maini yake utakuta magumu kama jiwe," alisema Mollel.

“Kwa ngo’mbe wanaokamuliwa maziwa yake yanapoteza ladha yake na kuwa machungu.”

Mwenyekiti wa kijiji cha Bwawani, Frank Mollel, alisema majani hayo yamesababisha madhara kwa watu 69 kuathiriwa baada ya kuyashika kwa mikono.

“Wananchi wangu wamelala ndani kutokana na athari za majani haya, hawawezi kufanya kazi yoyote, hivyo ni jukumu letu kwa kushirikiana na serikali kupambana na janga hili,” alisema.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake, Amina Shabani, aliiomba serikali kuwekeza nguvu za dhati kwenye kupambana na mmea huo.

“Ukiangalia mashamba yote utaona kuwa jani hili ndilo limeshamiri kwa kasi wakati huo linadhulu mazao yetu,” alisema. 

Habari Kubwa