TPSF yakoleza moto vita ya corona

24Mar 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
TPSF yakoleza moto vita ya corona

KATIKA juhudi za kuhakikisha kuwa maambukizi ya ugonjwa wa corona hayaenei na kuleta madhara katika sekta mbalimbali za uchumi nchini, Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), imeunda kamati maalum ya kushughulikia suala hilo.

Kaimu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Angelina Ngalula, akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, kuhusu masuala mbalimbali ya kujilinda na maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa corona likiwamo la kulinda biashara na ajira za Watanzania. PICHA: MIRAJI MSALA

Aidha, Taasisi hiyo imekuja na vipaumbele vyake vitatu kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa TPSF, Angelina Ngalula, alisema sekta binafsi imeguswa na kutambua kazi kubwa inayofanywa na serikali katika kukabiliana na ugonjwa huo, hivyo sekta binafsi hainabudi kuunga mkono juhudi hizo kwa vitendo.

“Tunapenda kutambua jitihada za Rais John Magufuli, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, kwa kuweka mikakati mahususi ya kupambana na ugonjwa huu na kuhakikisha tunajiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa kiafya, kijamii na kiuchumi,” alisema Ngalula.

Ngalula alisema TPSF kupitia kamati yake imejipanga kutoa elimu kwa umma kuhusu maambukizi, kujikinga na kudhibiti ugonjwa huo kulingana na muongozo na maelekezo yaliyotolewa na serikali kupitia Wizara ya Afya.

“Taasisi itashirikiana na wadau wa sekta kuhakikisha jamii ya Tanzania inapata taarifa sahihi katika maeneo yote matatu yaani
maambukizi, kujikinga na kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo,” alisema na kuongeza kuwa Kamati ilishakutana na Waziri wa Afya na Naibu wake.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, kazi ya pili ya kamati hiyo itakuwa kushirikiana na wadau kufanya uhamasishaji wa upatikaji wa rasilimali zinazohitaji katika kudhibiti maambukizi na athari za ugonjwa.

“Pamoja na mambo mengine, kamati iliyozungumza na Waziri Mwalimu na Naibu wake, Dt. Faustine Ndungulile, kuhusu vifaa vinavyohitajika kama vilivyoainishwa na Waziri wa Afya ni pamoja na (maski, sanitizers, protective gowns, ventilators, ambulance, scanners kama walk-through scanners na oxygen materials,” alisema.

Ngalula aliitaja kazi ya tatu ya kama hiyo ni kulinda ajira za Watanzania ambapo alisema TPSF kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameshaanza kujadili na kupanga mikakati ya kuona namna bora ya kulinda ajira za watu, biashara na uzalishaji.
“Tunapenda kuunga mkono taarifa aliyoitoa Mheshimiwa Rais Ana (Jumapili) kupitia vyombo vya habari kuwatoa hofu Watanzania na kuwaomba waendelee na kazi, huku wakichukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo,” alisema.

Ngalula alisema TPSF kupitia kamati yake, imeshafanya mambo mengi ikiwamo kuanza zoezi la kufanya tathmini ya awali ya athari za COVID-19 kwenye sekta mbalimbali za kiuchumi.

“Tayari wadau mbalimbali wa sekta binafsi wameshatoa majengo kwa ajili ya kuwahifadhi baada ya wasafiri wenye maambukizi kama sehemu ya kujitenga kwa muda wa wiki mbili,” alisema.

Kwa upande wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA), alisema wamehamasisha wanachama wake kutoa elimu ya maambukizi, kinga na udhibiti wa ugonjwa huo kwa madereva na wasaidizi wao.

“Tumeshahamasisha viongozi wote wa kongani 14 za taasisi kutoa elimu kwa wanachama wao katika kongani husika juu ya ugonjwa huo sambamba na mwongozo wa Wizara ya Afya,” alisema.

Habari Kubwa