TPSF yataka ubia na wawekezaji

07Apr 2017
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
TPSF yataka ubia na wawekezaji

MWENYEKITI wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Dk. Reginald Mengi, amewataka wawekezaji kuja nchini kwa wingi kuwekeza na ikiwezekana kuingia ubia na sekta binafsi katika miradi mbalimbali, ikiwamo ya umeme ili kutimiza ndoto ya kufikia uzalishaji wa megawati 10,000 ifikapo 2040.

MWENYEKITI wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Dk. Reginald Mengi.

Dk. Mengi aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati wa kongamano la biashara kati ya Tanzania na Ufaransa.

“Tanzania ndio chaguo zuri la uwekezaji. Maeneo ya kuwekeza ni kwenye sekta ya nishati ambayo Tanzania hivi sasa ina watu wanaofikia milioni 50… kwa sasa inazalisha nishati ya umeme megawati 1,500 na inahitaji dola za Kimarekani bilioni 46.2 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya nishati ya umeme ili iweze kuzalisha takribani megawati 10,000 ifikapo mwaka 2040,” alisema.

Dk. Mengi alisema uwekezaji hutegemewa zaidi kutoka sekta binafsi, hivyo, ni nafasi ya wazi kwa wawekezaji wa nje kuungana na wazawa katika kuchangamkia fursa zilizopo.

Aidha, alisema pamoja na ukweli kwamba Tanzania ina fursa kwenye masoko ya Ufaransa kupitia makubaliano ya sasa ya mpango wa GSP unaoruhusu vitu vyote kuuzwa nje isipokuwa silaha, lakini mauzo hayajazidi dola milioni 100.

Alisema mwaka 2015, asilimia 90 ya mauzo kwenye soko la Ufaransa kwa bidhaa za Tanzania yalitokana na bidhaa za kilimo.

“Sekta binafsi ndiyo msingi wa maendeleo ya uchumi wa Tanzania kwa sababu ndiyo ambayo inakuza uchumi na kutoa ajira. Kwa hiyo, bila ya kuwekeza kwenye sekta hii, suala la kuondoa umaskini haliwezi kufikiwa... kwa hali hii inabidi tuwe na sekta binafsi yenye nguvu,” alisisitiza.

Dk. Mengi aliwaondoa woga vijana kwa kuwaeleza kuwa hata kama hawana fedha, bado wanaweza kuwa wabia katika biashara kupitia ujuzi walionao.

“Vijana wa Tanzania wamekuwa hawajiamini. Kila mmoja anasema hawezi. Lazima vijana mseme mnaweza. Mitaji yenu ni nguvu, uwezo na ujuzi… mnaweza kushirikiana na wenzenu na kufanikiwa. Umaskini ni changamoto, kila siku sema ninaweza. Mimi nilizaliwa kwenye nyumba ya udongo, lakini leo nimefika hapa.

“Tusisubiri tuwe na fedha mfukoni ndio tuwe na ushirikiano kwenye biashara. Siyo kila mtu mwenye biashara ana pesa. Wengine ni uwezo walionao. Ni matumaini yangu nyie mliopo hapa siku moja mmoja wenu atanipa lifti kwenye ndege yake kwenda Kilimanjaro,” alisema.

Aidha, aliipongeza serikali chini ya Rais John Magufuli kwa kutengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya kufanya biashara.

“Mfano, bajeti ya mwaka uliopita serikali ilijikita kushughulikia masuala yanayozuia kukua kwa viwanda nchini ambayo ni kutokuwa na maji na umeme wa uhakika, usafirishaji na kuongeza uzalishaji kwa mazao ya kilimo ambayo yatatumika kama malighafi kwenye viwanda,” alisema.

Pia alisema serikali imeshughulikia tatizo la rushwa na ukiritimba usio wa maana katika kufikia maamuzi yenye tija.

Aidha, Dk. Mengi alisema ukuaji wa biashara ndogo na za kati ni muhimu katika mazingira ya biashara kati ya Tanzania na Ufaransa.

Balozi wa Ufaransa nchini, Malika Berak, alisema kwa mara ya kwanza Tanzania na Ubalozi wa Ufaransa wameandaa kongamano hilo kwa kushirikiana na kampuni 40 za Ufaransa na wadau kutoka sekta ya umma na binafsi.

Alisema ushiriki katika kongamano hilo ni muhimu na litapanua wigo wa ufahamu wa shughuli mbalimbali za nchi hizo mbili ikiwa ni pamoja na kufahamu mahitaji ya Tanzania katika masuala ya maendeleo na ujuzi wa kampuni za Ufaransa.

Mkurugenzi wa TPSF, Godfrey Simbeye, alisema kuna nafasi kubwa za kampuni za Kitanzania kuwekeza Ufaransa.

“Katika jukwaa hili, kampuni zilizokuja Tanzania zinaweza kutoa fursa kwa kampuni zetu kuwezesha sehemu ya shughuli kufanyikia Tanzania. Habari njema ni kwamba Ufaransa wapo tayari kushirikiana na kampuni za Tanzania na wanasema hawawezi kufanya wenyewe,” alisema.

Alisema kampuni za ndani zinatakiwa kuchangamkia fursa hiyo kwa sababu Ufaransa wamepiga hatua kwenye maeneo mbalimbali yakiwamo ya kilimo, magari na ndege.

Katika kuimarisha ushirikiano na urafiki kati ya nchi hizo mbili, juzi Dk. Mengi ambaye pia ni Mwenyekiti wa IPP aliwaandalia chakula cha jioni wafanyabiashara wa Ufaransa walioongozana na Balozi Malika.

 

Habari Kubwa