TRA Manyara yajipanga kuandikisha walipa kodi wapya 24,000

12Jan 2019
Jaliwason Jasson
Babati
Nipashe
TRA Manyara yajipanga kuandikisha walipa kodi wapya 24,000

MAMLAKA ya Mapato nchini (TRA), mkoani Manyara inatarajia kuandikisha walipa kodi wapya 24,000 ndani ya miezi sita ijayo, zoezi litakalohusisha mamlaka zote za kiutawala kuanzia ngazi ya chini kabisa hadi juu.

Meneja wa TRA mkoani hapa, Joseph Mtandika, alisema hayo wakati akizungumza na Nipashe ofisini kwake kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu ulipaji wa kodi kwa mujibu wa sheria za kodi.

“Tutapita kitongoji kwa kitongoji, kijiji kwa kijiji, kata kwa kata, tarafa kwa tarafa na mji kwa mji kuandikisha walipa kodi wapya ili tuwatambue na tuongeze wigo wa walipa kodi kwa kila anayestaili kulipa kodi na alipe,’’ alisema.

Alisema programu hiyo itakayotekelezwa mkoani hapa itafanyika pia nchi nzima kuanzia Januari hadi Juni, mwaka huu.

“Lengo ni kuhakikisha kila mtu anayestaili kulipa kodi ya serikali analipa kwa wakati uliopangwa na kodi hiyo iweze kuifikia serikali ili ijenge miundombinu ya huduma za kijamii.

Nipashe ilitaka kujua wafanyabiashara wanaoomba kulipa madeni yao kwa awamu wamewekewa utaratibu gani ambapo alisema sharti la kwanza atalipa na adhabu kwa kuwa ameikopa serikali.

“Mfano umekuja tumekubaliana namna utakavyolipa ila siyo utuambie utalipa kwa miaka mitano labda umetuambia utalipa mfululizo kwa miezi minne ukianza kulipa mwezi wa kwanza, wa pili, wa tatu ukaacha unafutiwa ule msamaha wote na ukirudi inabidi ulipe yote kwa kuwa umekiuka makubaliano,’’ alieleza

Alifafanua walipa kodi wa namna hiyo ambao wanakiuka makubaliano ya ulipaji kupitia njia ya msamaha huwa wakirudi mara ya pili hawana msamaha badala yake wanatakiwa kulipa kodi yote kwa wakati mmoja.

Aliongeza idadi ya wafanyabiashara wanaofuata masharti ya msamaha huwa inalingana kwa asilimia 50 kwa 50 na wale wafanyabiashara wasiofuata masharti ambao wanakiuka makubaliano ambayo yanawapa mwanya wa kulipa madeni yao kwa awamu ili waendelee kuwa na uhalali wa kufanya biashara zao.

Wakati huo huo, alisema kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Julai 2018/19 hadi Desemba, wameshakusanya mapato ya asilimia 105 na kuvuka malengo.

Alisema mkoa huo ni miongoni mwa mikoa minane mpaka 10 inayofanya vizuri kwa ukusanyaji wa mapato kitaifa.

Alipoulizwa siri ya mafanikio, alisema ni ushirikiano uliopo na vyombo vya ulinzi na usalama, utendaji kazi wa watumishi na kujituma.

Aidha alisema kwa mfano, msimu wa utalii kwa kipindi cha Julai hadi Novemba ulikuwa mzuri hivyo, hoteli nyingi za kitalii zililipa kodi ya ongezeko la thamani kama zinavyotakiwa na kiwanda cha sukari cha Manyara kililipa kodi ya ongezeko la thamani kuanzia Juni hadi Desemba, hivyo serikali ikapata mapato yake na mkoa ukapaa na kufikia malengo.

Alitumia fursa hiyo kuwataka wafanyabiashara kuwa wazalendo huku akiwataka kuitumia siku ya Alhamisi ya kila wiki kufika ofisi za TRA kuongea na meneja wa wilaya au mkoa kwa wale wenye malalamiko kuhusu kodi au wanaotaka kuanzisha biashara kuuliza namna wanavyoweza uanza biashara.

Hata hivyo, alisema utaratibu wa wateja wao kuonana na mameneja ulikuwepo lakini sasa kwa nchi nzima utakuwa Alhamisi.

Lakini alisema, wateja wakija siku zingine za wiki hawatazuiliwa kuonana na meneja huyo husika.