TRA sasa yapanga upya mnada nyumba za Lugumi

22Apr 2018
Beatrice Shayo
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
TRA sasa yapanga upya mnada nyumba za Lugumi

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imesema inajipanga kuziuza upya kwa mnada nyumba za kifahari za mfanyabiashara, Said Lugumi.

nyumba Ya Lugumi

Mfanyabiashara huyo anadaiwa kodi ya Sh. bilioni 14 na Mamlaka hiyo na Kampuni ya Udalali ya Yono, ndiyo iliyopewa kazi ya kupiga mnada nyumba hizo tatu.

Nyumba mbili kati ya hizo ziko Mbweni karibu na kambi ya JKT na moja iko Upanga mtaa wa Mazengo.

Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema ni mapema mno kuzungumzia lini wamepanga kuziuza upya.

 “Hizi nyumba bado zipo mikono mwa dalali, utaratibu mpya utapangwa na zitauzwa kwa wakati mwafaka kwasababu bado hazijauzwa. Wakati ule hakupatikana mnunuzi aliyefikia bei elekezi hivyo zitanadiwa tena,” alisema Kayombo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yono, Scholastika Kevela, alisema wamejipanga, lakini wanasubiri maelekezo kutoka kwa TRA.

“Mimi siyo msemaji kwenye jambo hili, nashauri ni vizuri ukawatafuta TRA ila kwa upande wetu tunajipanga taarifa kamili utapatiwa huko,” alisema.

Awali, kwenye mnada wa kwanza wa Novemba 9, mwaka jana, mnunuzi aliyetambulika kwa jina maarufu la Dk. Shika, aliibuka kidedea baada ya kutangaza dau la Sh. bilioni 3.3 kwa nyumba zote tatu.

Hata hivyo, Dk. Shika aliishia mikononi mwa polisi baada ya kubainika hakuwa hata na senti tano kulipia walau asilimia 25 ya dau aliloahidi kama taratibu za mnada zinavyotaka.

Baadaye Dk. Shika akajitwalia umaarufu mkubwa kutokana na tukio hilo, hasa kwa kauli yake ya ‘milioni 900 itapendeza zaidi’, akiashiria kuwa na uwezo wa kulipa kiasi hicho katika nyumba mojawapo.

Licha ya kusisitiza kuwa yeye ni bilionea anayesubiri fedha zake kutoka katika kampuni yake iitwayo Lancefort iliyopo Urusi, Dk. Shika hajamudu kulipa fedha hizo na baadaye ilibainika anaishi kwenye chumba kimoja cha kupanga, eneo la Tabata Mawenzi, jijini Dar es Salaam.

Baada ya mnada huo kukwama ilipangwa tarehe nyingine kwa ajili ya mnada wa pili ambao ulifanyika Novemba 24, mwaka jana na hakupatikana mteja wa kuzinunua.

Nipashe ilimtafuta Dk. Shika ili kufahamu kama atashiriki katika mnada huo na kusema kwa sasa hayupo tayari kulizungumzia suala hilo kwa kuwa kuna umbeya mwingi unaoendelea.

Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd., iliyotajwa katika sakata la zabuni ya Sh. bilioni 34 ya kuweka mashine za kielektroniki za kuchukua alama za vidole ya Jeshi la Polisi, na inadaiwa kodi na TRA na kusababisha mali zake zipigwe mnada.

Lugumi ilikuwa gumzo mwaka juzi baada ya taarifa ya CAG kuonyesha kuwa ililipwa zaidi ya asilimia 90 ya fedha za zabuni kwa ajili ya kuweka vifaa hivyo katika vituo 138, lakini hadi wakati wa ukaguzi ilikuwa imeweka katika vituo 14 tu.

Taarifa hiyo ilifika bungeni na kuundwa kamati ndogo ambayo ilichunguza na kuwasilisha taarifa.

Habari Kubwa