TRA yaibuka tena kusaka risiti za EFD

03Sep 2017
Gurian Adolf
Nipashe Jumapili
TRA yaibuka tena kusaka risiti za EFD

MAMLAKA ya Mapato (TRA) mkoani Rukwa jana imefanya msako kwa lengo la kukagua mabasi ya abiria pamoja na ya mizigo ambayo hayajalipiwa kodi.

Katika ukaguzi huo mamlaka iliangalia iwapo yanatumia risiti za kielekitroniki EFD wanapojaza mafuta katika vituo vinavyouza mafuta.

Msako huo ulianza saa 11:30 alfajiri katika stendi kuu ya mabasi iliyopo mjini Sumbawanga kwa kukagua mabasi yanayotoka mjini Sumbawanga na kuelekea sehemu mbalimbali za wilaya za mkoa huo pamoja na mabasi yanayosafiri mikoani.

Akizungumza wakati akiongoza msako huo Meneja Msaidizi Idara ya Ukaguzi wa TRA mkoa huo, Amina Shamdas, alisema kuwa mamlaka hiyo inashirikiana na kampuni ya madalali ya Yono Auction Mart kufanya ukaguzi huo.

Alisema mamlaka hiyo ilibaini wafanyabiashara wa usafirishaji hawadai risiti zinazotolewa na mashine za EFD wakati wakinunua mafuta.
Pia magari mengi yana stika za kulipia mapato za kughushi ndiyo sababu waliamua kufanya msako huo.

Alisema kuwa kufuatia msako huo anaamini wafanyabiashara hao watabadilika na kuanza kufuata sheria zilivyo ili waweze kuepukana na mkono wa sheria vinginevyo watajikuta katika wakati mgumu pindi wanapofanya biashara zao.

Meneja huyo alisema kuwa ifike wakati kila mwananchi aone fahari kulipa kodi kwani kwa kufanya hivyo atakuwa ametimiza wajibu wake kwa taifa na hatopata usumbufu wowote katika shughuli zake.

David Philipo, mwakilishi wa kampuni ya Action Mart ya mjini Sumbawanga, aliyeshiriki kwenye msako huo , alisema kuwa wamekuwa wakikutana na changamoto kubwa kutoka kwa wafanyabiashara hao ambapo baadhi yao ni wakaidi kutii sheria.

Alisema kwa kuwa wamejipanga vizuri kwa kushirikiana na TRA watahakikisha hakuna mapato yatakayopotezwa kwa ujanja kwa vile ni lazima serikali ikusanye kikamilifu kodi ili iweze kuwahudumia wananchi wake wakiwamo wasafirishaji ambao wanatumia huduma za barabara zinajengwa kwa kodi.

Habari Kubwa