TRA yaja na kampeni ‘mlango kwa mlango’

16Sep 2020
Halima Ikunji
Tabora
Nipashe
TRA yaja na kampeni ‘mlango kwa mlango’

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imekusudia kuwafikia wafanyabiashara 3,500 katika kampeni ya elimu ya mlipakodi maarufu ‘mlango kwa mlango’.

Meneja wa Elimu ya Mlipakodi wa TRA Makao Makuu, Diana Masalla:PICHA NA MTANDAO

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana, Meneja wa Elimu ya Mlipakodi wa TRA kutoka makao makuu, Diana Masalla, alisema lengo la kutoa elimu hiyo ni kuwajengea uelewa wa wafanyabiashara na walipakodi masuala  yanayohusu kodi.

Alisema kampeni hiyo inalenga kuwaondoa hofu wafanyabiashara ili wasiwaone maofisa wa TRA kama ni watu wanaowakomoa bali lengo ni kuwa marafiki ili waweze kulipakodi kwa hiari yao wenyewe.

Maofisa hao wanatoa elimu hiyo na kusikiliza maoni ya wafanyabiashara kwa ajili ya kuboresha huduma za TRA na kuwakumbusha kulipa kodi stahiki na kwa wakati.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk. Philimon Sengati, alisema kwamba wananchi na wafanyabiashara wanapolipa kodi ndio kichwa cha uchumi wowote duniani.

Alisema kutokana na jitihada kubwa za serikali za kukusanya kodi, ndio maana miradi mikubwa inatekelezwa nchini kwa kuwa ni kodi za Watanzania wenyewe zinafanya kazi hiyo.

Dk. Sengati alisisitiza kwamba serikali inatumia gharama kubwa kuendeleza huduma za kijamii ikiwamo ujenzi wa vituo vya afya, zahanati, barabara, madaraja na elimu bure kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Aliwataka maofisa wa TRA kuacha kutumia nguvu kwa ajili ya kukusanya kodi bali watumia elimu hiyo pamoja na lugha nzuri kwa wafanyabiashara hao.

“Sote tunafahamu umuhimu wa kodi katika maendeleo ya nchi yetu na ni ukweli usiopingika tumeona jinsi kodi inavyofanyakazi katika kipindi hiki cha serikali ya awamu tano inayoongozwa na Dk. John Magufuli,” alisema Sengati.

Habari Kubwa