TRA yataifisha bidhaa za zaidi ya mil. 84/-

02Nov 2017
Mary Mosha
Nipashe
TRA yataifisha bidhaa za zaidi ya mil. 84/-

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Kilimanjaro, imeingiza Sh. milioni 84.7 baada ya kutaifisha bidhaa za magendo zilizoingizwa nchini kinyume na sheria na kuziuza.

Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro, Msafiri Mbibo.

Bidhaa hizo zikwamo mafuta ya taa na dizeli zilikamatwa katika kipindi cha Julai 2016 hadi Disemba 2016, lita 67,599 zilizoingia nchini kwa kupita njia zisizo rasmi yakitokea nchi jirani ya Kenya.

Hayo yalibainishwa jana na Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro, Msafiri Mbibo, wakati akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu hali ya uingizwaji wa bidhaa mbalimbali kutoka nchi jirani ya Kenya kwa njia za magendo.

“TRA kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, tumekuwa tukifanya kazi ya kuzuia uingizwaji wa bidhaa nchini kutoka nje ya nchi kwa kupitia njia za magendo, na katika operesheni zetu tumefanikiwa kukamata mafuta ambayo tuliyauza na kupata zaidi ya Sh. milioni 84.7,” alisema.

Mamlaka hiyo pia ilikamata vyombo vya usafiri vilivyokuwa vikitumiwa kusafirisha mafuta hayo ambavyo ni pikipiki 20 na magari mawili yanayosubiri taratibu za kiforodha ili vyombo hivyo viweze kupigwa mnada.

Mbibo alisema katika Mkoa wa Kilimanjaro, ipo changamoto kubwa ya mpaka kuwa mkubwa, huku vituo vya TRA vikiwa viwili pekee, hali ambayo inawafanya wafanyabiashara wasio waaminifu kubuni njia zisizo rasmi na kupitisha bidhaa mbalimbali kuingiza nchini kinyume cha sheria.

“Mpaka wetu wa Kenya na Tanzania ni mkubwa, kwa sasa wafanyabiashara wengi hutumia usafiri wa pikipiki kuvusha bidhaa kutoka nchi jirani ya Kenya na kuingiza nchini, lakini naomba wafanyabiashara watambue kuwa, pamoja na changamoto hiyo, tumejipanga vizuri na wote watakaokamatwa, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kutaifisha bidhaa na chombo cha usafiri alichokuwa akitumia,” alisema.

Aliwataka wafanyabiashara nchini kuwa wazalendo na kuepuka biashara za magendo ambazo zinachangia kudidimiza na kuua soko la ndani.

“Bidhaa kama mafuta ya taa wanayoingiza nchini kwa njia za magendo yakifika huuza kwa bei chee, bei ambayo haiwezi kushindana na bidhaa iliyoko nchini, hivyo ni vyema wafanyabiashara wakauvaa uzalendo ili kuweza kulinda soko la ndani la bidhaa hiyo,” alisema.

Aidha Mbibo alisema katika kuhakikisha wanadhibiti biashara za magendo nchini, wanashirikiana na viongozi wa serikali za mitaa na vijiji kutoa elimu katika maeneo mbalimbali hususani ya mipakani, lengo likiwa kuwawezesha wananchi wanaoishi maeneo hayo kuwa mabalozi wa kwanza katika kupinga uingizwaji wa bidhaa za magendo nchini.