TRA yawashtukia wafanyabiashara

19Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Kahama
Nipashe
TRA yawashtukia wafanyabiashara

BAADHI ya wafanyabiashara wilayani hapo, mkoani Shinyanga, wameanza kuandika barua za kuomba kuacha kufanyabiashara, kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), huku wengi wakiingia katika mfumo mpya wa vitambulisho vya wajasiriamali vya biashara ndogo ndogo.

Hayo yalibainishwa jana na Kaimu Meneja wa TRA Mkoa Maalumu wa Kikodi Kahama, Faustine Kayambo, wakati akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake kuwa kwa wale ambao hawana sifa ya kupata vitambulisho ni bora wakaendelea kufanyabiashara zao na kulipa kodi ya serikali.

Alisema mpaka sasa ni zaidi ya wafanyabiashara 100 ambao wameandika barua za kuomba kuacha biashara, kati ya hao mamlaka yake iliwatembelea wawili kujiridhisha na kuwakuta na bidhaa zenye thamani kubwa ambazo haziwafanyi kuingizwa katika mfumo wa kuwa na vitambulisho vya ujasiriamali.

"Kuna barua nyingi tayari ofisini kwangu na ninapokea idadi ya kuanzia barua nane hadi 10 kwa siku kutoka kwa wafanyabiashara za kuacha biashara zao, na ofisi yangu imebaini kuwa wengi wao wanakuwa na nia ya kukwepa kulipa kodi na kujiunga na vitambulisho vya wajasiriamali," Kayamba alisema.

Aliongeza: "Mpaka sasa Mamlaka imefanya msako kujiridhisha na hali hiyo na tuliwabaini wafanyabiashara wawili ambao wana vitambulisho vya wajasiriamali wadogo na tulifanikiwa kuwakamata na kuwanyang’anya na kuvirudisha kwa Mkuu wa Wilaya Anamringi Macha.

Alieleza kuwa walioandika barua za kuacha biashara majina yao yote yameorodheshwa na wanakadiriwa kuwa zaidi ya wafanyabiashara 80 hadi 100 na Mamlaka yake itawatembelea ikiwa ni pamoja na kuangalia kama wana madeni ya kodi katika siku za nyuma.

Hata hivyo, Kayambo alitoa wito kwa wanaostahili kulipa kodi ni bora wakaendelea kulipa kwa wakati na kama mitaji yao itakuwa imeyumba wanaweza kufika katika ofisi yake kwa lengo la kukadiriwa kodi upya huku akiwa katika uangalizi.

Pia alisema wenye mauzo chini ya shilingi milioni nne kwa mwaka, wanatakiwa kuendelea kuvitumia vitambulisho ambavyo vinatolewa na serikali ili kuepuka usumbufu baadaye.

Katika hatua nyingine, Kayambo alitoa onyo kwa wafanyabiashara ambao hawatoi risiti na ambao hawachukui risiti kuwa atawachukulia hatua za kisheria kwa kuwapiga faini ya shilingi milioni tatu hadi Sh. milioni 4.5 kwa ambaye hatoi risiti na Sh. 300,000 hadi Sh. milioni 1.5 kwa mteja ambaye atakuwa hajaomba risiti.

Habari Kubwa