TSN kujenga madarasa Shule ya Msingi Majimatitu

04Mar 2016
Mary Geofrey
Dar
Nipashe
TSN kujenga madarasa Shule ya Msingi Majimatitu

KAMPUNI ya Tanzania Sisi Nyumbani (TSN), kupitia taasisi yake ya TSN Foundation, imeahidi kujenga madarasa matano katika Shule ya Msingi Majimatitu jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki.

Vile vile, kampuni hiyo imejitolea kulea kituo cha watoto wenye mahitaji maalum kilichopo shuleni hapo.

Hayo yalisemwa na Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Abdul Ngomi, wakati akizungumza na Nipashe kuhusu msongamano wa wanafunzi katika shule hiyo.

“Tunaishukuru na kuipongeza kampuni ya TSN maana imeonyesha nia ya dhati ya kutusaidia. Tunaendelea na mazungumzo kuangalia jinsi gani watatuvusha katika hali hii ngumu,” aliongeza Ngomi.

Mbali na TSN, pia wafadhili mbalimbali wamejitokeza wakiwamo kutoka nchini Uturuki ambao wameahidi kujenga shule mpya mbili katika kukabiliana na mrundikano wa wanafunzi.

TSN Foundation kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki, wanaandaa mkakati wa kuwashirikisha wananchi wote wa mkoa huo kuondoa kero ya wanafunzi kukaa chini na ukosefu wa madarasa.

Shule ya Majimatitu ina wanafunzi 6,000, darasa la kwanza pekee wako 1,025 hali inayosababisha wengi wao kusomea chini ya miti.

Mwalimu Ngomi alisema Uturuki imekubali kujenga shule hizo katika eneo la Majimatitu `B' na nyingine kwenye kiwanja cha Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) ambacho kimechukuliwa na serikali.

Ili kukabiliana na tatizo hilo, shule hiyo inahitaji vyumba madarasa vya ziada 109, matundu ya vyoo 239 na lita za maji 32,000 kwa siku.

Hata hivyo, kwa sasa madarasa yaliyopo ni 22 tu, matundu 36 ya vyoo na maji yanayopatikana ni lita 8,000.

Akizungumza na wazeee wa Mkoa wa Dar es Salaam hivi karibuni, Rais John Magufuli, aliwapongeza wawekezaji wazalendo ambao wameahidi kusaidia ujenzi wa madarasa ili kuhakikisha wanafunzi hawakai chini.

Habari Kubwa