Tume yabaini matundu sheria ufilisi

15Jun 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Tume yabaini matundu sheria ufilisi

TUME ya Kurekebisha Sheria imependekeza kutungwa kwa sheria mahsusi itakayosimamia masuala ya ufilisi kutokana na kuwapo changamoto mbalimbali ikiwamo kutoa adhabu ndogo.

Rais Dkt. John Magufuli akizungumza jambo na Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Jaji Mstaafu January Msofe.PICHA MTANDAO

Pendekezo hilo limekuja baada ya kubaini kuwapo sheria za ufilisi ambazo zimepitwa na wakati na baadhi zinatoa adhabu au faini ndogo kwa wale wanaokiuka taratibu za ufilisi kama vile Sh. 200 au Sh. 1,000.

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji mstaafu January Msoffe, alisema hayo jana alipokuwa akiwasilisha ripoti ya mapitio ya sheria zinazosimamia mfumo wa ufilisi Tanzania kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Augustine Mahiga.

Jaji Msoffe alisema utafiti wao umebaini hadi sasa hakuna sheria mahsusi inayosimamia masuala ya ufilisi nchini.

Alisema masuala hayo yamekuwa yakisimamiwa na sheria mbalimbali za kisekta kama vile Sheria ya Kampuni sura ya 212, Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha Sura ya 342, Sheria ya Vyama vya Ushirika Sura ya 211, Sheria ya Ufilisi, Sheria ya Bima Sura ya 394, Sheria ya Mashirika ya Umma na Sheria ya Usajili wa Wadhamini Sura ya 318.

Mwenyekiti huyo alisema kuwapo kwa sheria hizo kunasababisha mkanganyiko kwa watumiaji kwa kutojua ni sheria ipi inayopaswa kutumika, ili kutatua tatizo linalowakabili.

"Kuwapo kwa sheria hizi kumesababisha ugumu kwa wadai kujua utaratibu wa kutumia kupata haki zao kwa wakati baada ya kampuni au taasisi husika kufilisika. Pia kumesababisha uwapo wa taratibu ndefu, hivyo kuchelewesha mashauri ya ufilisi kumalizika kwa wakati," alisema.

Alifafanua kuwa faini ambazo zimekuwa zikitolewa kwenye sheria hizo haziendani na kiwango cha kiuchumi cha maisha ya sasa.

"Baadhi ya sheria hizo, zinatoa kiwango kidogo sana cha mtaji ili kampuni au taasisi ionekane kuwa imefilisika. Pia sheria hizi zinatambua njia moja ya mawasiliano mfano kwa njia ya posta," alisema.

Jaji Msofe alisema hali hiyo inafanya sheria hizo kutoendana na maendeleo yaliyopo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, hivyo kuna haja ya kuzirekebisha ili ziendane na mazingira ya sasa.

KUFILISI KAMPUNI

Akizungumzia kuhusu ugumu wa taratibu za kisheria kwenye ufilisi wa kampuni za nje zenye kampuni tanzu Tanzania, Jaji Msoffe alisema utafiti wao umebaini masuala yanayosimamia ufilisi kwenye kampuni unasimamiwa na Sheria ya Kampuni, Sura ya 25.

Hata hivyo, alisema sheria hizo hazijaainisha kwa kina taratibu za ufilisi kwenye kampuni za nje zenye kampuni tanzu Tanzania tofauti na nchi za Kenya na Uganda ambazo zimeweka utaratibu mzuri wa kisheria unaoweza kufuatwa katika ufilisi huo.

Pia alisema utafiti wao umebaini Tanzania vipo vyombo mbalimbali kwa mujibu wa sheria vinavyoweza kusimamia masuala hayo kama vile kuangalia mali za kampuni au taasisi pale inapofikia hatua ya kufilisiwa.

Pamoja na kuwapo kwa mamlaka hizo, alisema hakuna kanzi data ambapo mamlaka hizo zinaweza kupata taarifa za masuala ya ufilisi ili kuweka mazingira wezeshi kwenye biashara na uwekezaji.

Mashauri kuchelewa

Jaji huyo alisema utafiti umebaini kwamba mahakama zinakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinasababisha ucheleweshaji wa usikilizaji na kumalizika kwa mashauri kwa wakati.

"Mfano, shauri ya Tritel tangu kufunguliwa kwake mahakamani mwaka 1999 hadi leo halijaisha," alisema.

Kadhalika, alisema wamebaini kwa mujibu wa Sheria za Tanzania kampuni inapofilisika wanaopewa kipaumbele kulipwa haki zao ni walio na madeni ya kipaumbele na si wafanyakazi.

Kuhusu haki ya waweka akiba, Mwenyekiti huyo alisema wamebaini kwa mujibu wa Sheria za Tanzania benki inapofilisika wanapewa kipaumbele walio na madeni na si waweka akiba.

Kutokana na changamoto hizo, alisema tume hiyo inapendekeza kutungwa kwa sheria ya ufilisi ili kuondoa changamoto hizo ambayo pamoja na mambo mengine itaanzisha baraza la kutatua masuala hayo.

Habari Kubwa