Uagizaji bidhaa nje kupungua

09Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Singida
Nipashe
Uagizaji bidhaa nje kupungua

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema serikali itaendelea kupunguza uagizaji wa baadhi ya bidhaa zinazozalishwa nje.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, picha mtandao

Badala yake amesema ununuzi wa bidhaa zinazozalishwa ndani utaongezwa ili kukuza viwanda vya ndani hususan bidhaa za mbao na mafuta ya kula.

“Napenda kuwahakikishia kuwa, bidhaa zetu ni nzuri na zinapendwa na watu wengi hata wa nje ya nchi. Mnachotakiwa kukifanya ni kuzalisha bidhaa kwa wingi na kwa kutumia malighafi zinazopatikana kwenye maeneo yenu, hii itawezesha kuwa na uzalishaji wenye gharama ndogo na kuwa na bei shindani katika soko."

Waziri Mkuu ameyasema hayo juzi wakati akifungua Maonyesho ya Shirika la Viwanda Vidogo (Sido) kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya Bomberdia Manispaa ya Singida.

Alisema serikali itaendelea kujenga mazingira mazuri ya kuwa na viwanda vya kuongeza thamani ya madini nchini.

“Niwasihi Watanzania wote hasa wale wanaofikiria kuwa bidhaa zinazotoka nje ya nchi ndizo zenye ubora kuliko za hapa nchini, kuachana na dhana hiyo potofu, kwani bidhaa zetu ni bora na zina viwango vinavyostahili.”

Alisema wakizalisha bidhaa kwa kutumia malighafi za ndani itawezesha ajira endelevu kuwapo kwa vijana, itasaidia malighafi kutoharibika lakini bidhaa zitakazozalishwa zitakuwa na thamani kubwa badala ya kuuza malighafi kwa bei ya chini.

Pia Waziri Mkuu alisema serikali imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda ili kuifikisha nchi kwenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.

Alisema uanzishwaji wa viwanda umejikita zaidi katika uongezaji wa thamani wa mazao ya kilimo na maliasili yanayopatikana nchini, kama kilimo, mifugo, misitu, uvuvi na madini kwani wananchi wengi wanategemea mazao na rasilimali hizo kwa maisha yao.

Waziri Mkuu alisema serikali itaendelea kuhimiza uongezaji thamani wa mazao husika kwa kuwa ndiyo njia sahihi. “Kwa misingi hiyo, usindikaji, uchakataji na uchenjuaji, vitachangia kupunguza upotevu unaotokea msimu wa mavuno, kuongeza ajira na thamani ya mazao kwa lengo la kuwapatia wazalishaji kipato.”

Alisema uongezaji thamani utahitaji teknolojia (mashine na ujuzi), ambapo baadhi ya teknolojia hizo zimeonyeshwa kwenye maonyesho hayo.

“Vilevile maonyesho hayo yametoa fursa ya kuonyesha teknolojia zinazoweza kurahisisha uzalishaji na kuleta ufanisi zaidi ili kuongeza tija na kuhimili ushindani katika soko la ndani na nje.”

Mapema akitoa taarifa kuhusu maonyesho hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa SIDO, Prof. Elifas Bisanda, alisema wamekuwa wakiandaa maonyesho hayo ili kuwahamasisha wajasiriamali wadogo na wa kati wapate mbinu mpya juu ya viwanda vidogo.

Habari Kubwa