Uchunguzi mafuta, gesi wakamilika

05Dec 2017
Rahma Suleiman
Nipashe
Uchunguzi mafuta, gesi wakamilika

MKURUGENZI Mwendeshaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi asilia, Omar Zubeir, amesema uchunguzi wa utafutaji wa rasiliamali hiyo katika eneo la bahari yenye maji ya kina kirefu limefanikiwa licha ya kujitokeza changamoto.

Akizungumza na waandishi wa habari, alisema uchunguzi huo umeonyesha matumaini ya kupatikana kwa mafuta.

Alisema uchunguzi ulianza Oktoba 28 na kumalizika Novemba 28, mwaka huu.

Alisema idadi ya mistari iliyofanyiwa utafiti ndani ya kitalu cha Pemba ilikuwa 62, huku idadi ya kilomita zilizofanyiwa utafiti ndani ya kitalu cha Pemba zilikuwa 2,482.

Aidha, alisema idadi ya mistari iliyofanyiwa utafiti nje ya kitalu cha Pemba, Zanzibar ilikuwa ni minne huku idadi ya kilomita zilizofanyiwa utafiti nje ya kitalu cha Pemba, Zanzibar zilikuwa 333.6.

Alisema kuwa katika uchunguzi huo changamoto zilizojitokeza ni kuwapo kwa wavuvi katika baadhi ya maeneo ambao walisababisha uchunguzi kusimama kwa muda ili kupisha shughuli za uvuvi.

Aidha, alisema kumekuwapo na athari kwa baadhi ya nyavu za wavuvi kuharibiwa ambazo mamlaka imeahidi kulipa fidia.

"Hatua tulizozichukua ni kuhakikisha mkandarasi analipa fidia kwa uharibifu ulioripotiwa kwa mamlaka licha ya kuwa hakukuwa na idadi kubwa ya wavuvi waliojitokeza na kwa sasa tumekuwa na mtu mmoja tu ndie aliyejitokeza," alisema.

Kwa upande wa mtetemo kwa eneo la bahari ya maji ya kina kirefu, alisema limemalizika na sasa unatarajiwa kufanyika katika nchi kavu.

Alisema uchunguzi huo unatarajiwa kuanza karibuni na utachukua zaidi ya miezi saba na elimu itatolewa kwa wananchi wa maeneo hayo kwa ushirikiano wa masheha na kuahidi kuwalipa wananchi fidia watakaoathirika.