UDSM yabariki viwanda saba

26Jun 2017
Salome Kitomari
Aliyekuwa SIMIYU
Nipashe
UDSM yabariki viwanda saba

MKOA wa Simiyu umejipanga kujenga viwanda saba ambavyo vitatumia malighafi ya ndani na kutoa ajira kwa Watanzania.

Hayo yamebainishwa juzi mjini Maswa na Mtafiti kutoka Taasisi ya Mambo ya Kijamii na Kiuchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (ESRF), Dk. Gratian Bamwenda, wakati akiwasilisha taarifa ya upembuzi yakinifu ya upanuzi wa kiwanda cha chaki kupitia ujenzi wa uchumi wa viwanda Simiyu (SODIP).

Mpango huo wenye kauli mbiu ya 'bidhaa moja wilaya moja' ulibuniwa na mkuu wa mkoa huo kwa kushirikiana na wataalamu mbalimbali ikiwamo Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), ambao walifanya utafiti katika mkoa huo kwa nia ya kuainisha maeneo yanayofaa kwa uwekezaji.

Dk. Bamwenda alisema mwongozo wa uwekezaji kwenye mkoa huo ulibainisha kuwa kuna fursa 26 za kuwekeza kwenye mkoa huo, lakini upembuzi yakinifu ulipofanyika, ilibainika saba ndiyo zinafaa kuanza kwa sasa.

Alitaja miradi hiyo kuwa ni upanuzi wa kiwanda cha chaki kinachozalisha katoni 400,000 kwa mwezi hadi milioni 1.2 ambazo zitaweza kutumika kwenye shule za msingi na sekondari 22,260, na kuuzwa kwenye nchi zaidi ya tano.

Mradi huo ambao umepewa fedha za upanuzi na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), unatarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja 100, na zisizo na moja kwa moja kati ya 500 hadi 800, huku kikitumia malighafi ya gypsum inayozalishwa Mkalama mkoani Singida.

Mradi huo unamilikiwa na Halmashauri ya Maswa kwa asilimia 95 na Maswa Family Group (kikundi cha vijana 16) kwa asilimia tano. Vijana hao wamepata ajira ya moja kwa moja na kutoa ajira kwa zisizo za moja kwa moja kwa wenzao kati ya 60 na 80.

Chaki zinazozalishwa na kiwanda hicho kwa sasa zinauzwa kwa kiasi kikubwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ambayo tayari imeshanunua katoni 2,530, ikifuatwa na Simiyu 1,806, Shinyanga 606, Geita 250, Tabora 100 na Mwanza 50 na kwamba toka kizinduliwe Oktoba mwaka jana, kimeshauza chaki za Sh. milioni 133.55.

Fursa nyingine ni kiwanda cha maziwa kinachotarajiwa kujengwa wilayani Meatu ambacho kitatumia malighafi ya maziwa kutoka kwa wafugaji.

Nyingine ni kiwanda cha tomaso na chili sauce kitakachojengwa wilayani Busega kikitumia malighafi ya ndani, kiwanda cha vifaa vya tiba kinachotarajiwa kujengwa wilayani Bariadi na kiwanda cha mazao ya ngozi na sabuni kitakachojengwa wilayani Itilima.

Mkuu wa mkoa huo, Antony Mtaka, alisema wamejipanga kutekeleza sera ya viwanda kwa vitendo kwa kuangalia viwanda vyenye kuleta matokeo chanya kwa wananchi na uchumi wa nchi.

"Tunachofanya ni kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya makundi ya vijana na wanawake zinapata maana kwa kuzipeleka kwenye miradi yenye matokeo chanya, na kwa kuanza walianza na cha chaki, kiwanda ambacho kimepata mkopo baada ya Serikali ya Zanzibar kukubali kununua chaki hizo," alisema.

"Tunaishukuru NSSF kwa imani kubwa, sisi tumedhamiria kuwa na bidhaa moja wilaya moja, mkoa mmoja kwa kiwanda kimoja, tunashukuru kwa UNDP kwa ufadhili wa upembuzi yakinifu kwa Wilaya za Busega, Meatu na Maswa.

"Kama halmashauri, tunakopa mabilioni kujenga soko au kituo cha mabasi kwanini tusikope kujenga viwanda vitakavyotumia malighafi zetu, vitakavyoajiri Watanzania na tutapata mapato?"

"Halmashauri za Mkoa wa Simiyu tunaamini kwa miaka mitano tutakuwa halmashauri za kipekee zenye miradi yake yenyewe ya kibiashara."
Alisema soko la Zanzibar limetoa nafasi kwa NSSF kuwaamini na kutoa mkopo kwa Sh. bilioni 1.5 ambao utapanua kiwanda hicho na kuzalisha katoni milioni 1.2 za chaki.

Mtaka alisema Rwanda ilitoka kwenye historia ya mauaji ya kimbari, lakini sasa inaheshimika duniani na anaamini mkoa wake wa Simiyu umetoka kwenye historia ya mauaji ya vikongwe na albino na sasa unakwenda kuheshimika kwenye uchumi.

Akipokea hundi ya mkopo huo kutoka NSSF, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alisema mfuko wa NSSF umejipambanua kutekeleza sera ya viwanda kwa vitendo kwa kuwekeza kwenye sekta hiyo katika viwanda vitakavyotumia malighafi za ndani na kuongeza ajira na wachangiaji kwenye mifuko hiyo.

Alisema atapeleka serikalini kilio cha wamiliki wa viwanda wazawa juu ya msamaha wa kodi ambao kwa sasa uko kwa wawekezaji wa kigeni pekee ili kuangalia namna ya kuondoa kikwazo hicho.

Waziri huyo alisema nia ya Rais John Magufuli ni kuingia kwenye uchumi wa viwanda vinavyofungamanishwa na maendeleo ya watu hasa watu maskini - kwamba viwe na uwakilishi wa matabaka yote na vinavyotumia malighafi ya ndani ambayo itaongeza mnyororo wa thamani.

"Kiwanda cha Maswa kimebeba ujumbe na dhana ya Rais ya kufungamanisha uchumi wa viwanda na maendeleo ya watu kwa kuwa kinatumia malighafi ya gypsum inayopatikana nchini, inatoka Mkalama Singida, faida itakuwa mara tatu au nne zaidi kuliko kutoa nje ya nchi," alisema.

Mhagama alisema zaidi: "Asilimia 56 ya nguvu kazi ni vijana ambao wengi wao hawana ajira, hivyo kiwanda hiki kitatumia malighafi ya ndani na kuwaajiri, vijana wa Mkoa wa Singida wanaoandaa malighafi wataajiriwa. Kinabeba dhana na matarajio ya Rais ya kuendeleza uchumi wa viwanda."

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Prof. Godius Kahyarara, alisema wapo watakaojitokeza kuwakatisha tamaa kuwa serikali haifanyi biashara, na kwamba duniani kote serikali inafanya biashara huku akitolea mfano wa nchi ya Ujerumani yenye mashirika ya umma 15,000, na Ethiopia ambayo kampuni yake ya simu ni moja ya kubwa zaidi duniani.

"Sisi ni shirika la umma, lazima tutekeleze sera na maelekezo ya serikali, suala la viwanda kwetu sisi ni kipaumbele, tutaendelea kushirikiana kwa kadiri iwezekanavyo kujenda viwanda vitakavyoleta mabadiliko kwenye maisha ya Watanzania wa kawaida," alissema.

Aliongeza kuwa NSSF itaendelea kushiriki ujenzi wa viwanda vitakavyobadili maisha ya Watanzania huku akiwataka wamiliki wa kiwanda hicho cha chaki kuzingatia miiko katika uwekezaji hasa soko na kuhakikisha gharama za uzalishaji zinashuka ili kutengeneza faida.

Habari Kubwa