Ufaransa yataja maeneo 9 ya ushirikiano na Tanzania

10Jul 2019
Salome Kitomari
Nipashe
Ufaransa yataja maeneo 9 ya ushirikiano na Tanzania

UBALOZI wa Ufaransa nchini Julai 14, mwaka huu, utasherehekea siku ya kitaifa, huku ukieleza maeneo tisa ya ushirikiano baina yake na Tanzania ikiwamo kuunga mkono jitihada za serikali kwenye mapinduzi ya uchumi.

Balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za Ubalozi huo jijini Dar es Salaam, Balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier, alisema siku hiyo inafahamika kama Bastille ikiwa ni kukumbuka Mapinduzi ya Ufaransa mwaka 1789.

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni haki za binadamu, kisiasa, uwekezaji na biashara, elimu, nishati, maji, kilimo, utalii na afya, ambayo nchi hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kuleta maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Balozi Clavier alisema Ufaransa inaunga mkono jitihada za Rais John Magufuli kuifanya nchi kuwa ya uchumi wa kati ifikapo 2025, na kwamba Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), litafadhili na kutoa kipaumbele kwa miradi ya maendeleo kwenye sekta za kipaumbele za nishati, usafiri na maji.

"Lengo letu ni kuhakikisha huduma muhimu na miundombinu kwa jamii katika maendeleo ya kiuchumi, tumeongeza zaidi ya mara mbili msaada wetu kwa Tanzania ambao umefikia mkopo wa Dola za Marekani milioni 110 kwa mwaka na Dola milioni 23 za msaada," alibainisha.

Kwa mujibu wa balozi huyo, mafanikio hayo yamedumu kwa miezi 12 na kwamba Septemba mwaka jana rais alizindua mradi wa maji wa Musoma uliogharimu Dola za Marekani milioni 27 ikiwa ni fedha kutoka AFD.

Pia alisema Bodi ya AFD imepitisha mkopo wa Euro milioni 100 kwa mradi wa umeme kati ya Zambia na Tanzania na kuongeza umeme kwenye gridi ya taifa.

Vile vile, alisema kuwa eneo la afya, nchi hiyo imetoa mkopo wa Dola za Marekani milioni 53 kwa ajili ya upanuzi wa hospitali ya Aga Khan kwa kuongeza vitanda 170 na vituo 27 nchini.

Kadhalika kwenye eneo la kilimo nchi hiyo itaendelea kusaidia miradi ya kijamii katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kupunguza umaskini na kwamba Dola milioni moja zimetolewa kwa wakulima wadogo 6,000 mkoani Mtwara.

"Biashara kati ya Tanzania na Ufaransa imeongezeka kwa asilimia 30 mwaka 2018 kwa thamani ya Dola za Marekani milioni 200. Umoja wa wafanyabiashara wa nchi hizi watakutana mwezi ujao katika mkutano utakaoleta pamoja kampuni 40 za Ufaransa zinazofanyakazi nchini," alisema na kuongeza:

"Ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Tanzania uko katika maandalizi ya mwisho kwenda Ufaransa ikiwa ni matokeo ya ujio wa ujumbe wa wafanyabiashara 35 kutoka nchini humo waliotembelea mwaka jana kuangalia uwezekano wa uwekezaji."
Kwa upande wa elimu, alisema kuna shule ya misngi iliyojengwa na kwa elimu ya juu wameendelea kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), ikiwa ni pamoja na kutoa ufadhili kwa wanafunzi kusoma nchini humo.

Awali, Mwenyekiti wa Tanzania wa Kampuni ya Total, Tarik Moufaddal, alisema kwa zaidi ya miaka 52 kampuni hiyo imewekeza kwenye maeneo mbalimbali ya sekta ya mafuta na kwamba kwa sasa wako kwenye mradi wa ujenzi wa bomba la Hoima nchini Uganda hadi Tanga, na kwamba wataendele kuunga mkono sera ya viwanda.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege la Swiss, Tanzania, Andre Bonjour, alisema kwa mwaka watu 25,000 kusafiri kutoka nchi mbalimbali duniani kuja Tanzania na kwa kiasi kikubwa kumesaidia kukuza sekta ya utalii.

Habari Kubwa