Ufuatiliaji kahawa kumpaisha mkulima

26Oct 2020
Restuta Damian
BUKOBA
Nipashe
Ufuatiliaji kahawa kumpaisha mkulima

UFUATILIAJI na usimamizi wa kilimo bora katika zao la kahawa utasaidia kunufaisha mkulima na kupata mafanikio ya tani 200,000 zitakazofikia asilimia 5 ya malengo ya soko la dunia.

kahawa.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Kahawa, Prof. Jamal Adamu, kwenye uzinduzi wa ugawaji miche ya kahawa kwa baadhi ya wakulima kutoka wilaya za Mkoa wa Kagera iliyozalishwa katika kitalu cha Gereza la Kitengule wilayani Karagwe na JJAD Kagera Farmers (T) LTD wilayani Kyerwa, lengo likiwa ni kusaidia mkulima kuongeza uzalishaji na kupata kipato.

Adamu alisema Bodi ya Kahawa kwa ushirikiano na kampuni ya JJAD Kagera Farmers, Cafe Africa inatenga miche milioni 20 kila mwaka kwa ajili ya kugawa kwa mkulima kama sehemu ya kujiongezea uzalishaji na kuendeleza kuingia katika masoko ya dunia.

"Bodi inaamini kuanzisha vitalu hivi viwili hapa mkoani ni malengo ya ongezeko la uzalishaji wa kahawa ya maganda, kwani mategemeo yaliyopo ni kufikia kuzalisha miche milioni 20 kwa mwaka ambayo itarahisisha Taifa kuwa na uongezaji wa tani 200,000 za kahawa,” alisema Prof.  Adamu.

Katibu Tawala mkoani Kagera, Prof. Faustine Kamuzora, alisema, kuanzisha mradi  wa miche uendane na aina tatu za wakulima na kuona hali ya uwezo wa kununua na kwamba  malengo ya pamoja ni kuona mkulima anapata kipato.

"Niseme tu miradi hii inayomlenga mkulima iangalie hata wale wa hali ya chini, kiwango cha kati na juu kwa sababu ujio wa miche hiyo umetokana na pesa inayotoka katika pato la wakulima wa aina zote na sio walio na hali ya juu,” alisema Prof. Kamuzora.

Habari Kubwa