Ujenzi kivuko cha Kayenze sasa kukamilika Novemba

19Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
MWANZA
Nipashe
Ujenzi kivuko cha Kayenze sasa kukamilika Novemba

UJENZI wa kivuko cha Kayenze kwenda Kisiwa cha Bezi mkoani Mwanza unaogharimu Sh. bilioni 2.7 unatarajiwa kukamilika Novemba mwaka huu.

Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akishuka kutoka katika kivuko cha Kayenze.

Hayo yalibainishwa juzi wakati Mbunge wa Ilemela mkoani Mwanza ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula, alipotembelea kivuko hicho kuangalia maendeleo ya ujenzi.

Kwa mujibu wa Mabula, kivuko hicho chenye uwezo wa kubeba abiria 250, magari 10 na ukubwa wa tani 10 kitaondoa kero ya muda mrefu waliyokuwa wakiipata wananchi wa Kayenze na Bezi.

“Wananchi wa Kisiwa cha Bezi na Kayenze Mwaloni wamekuwa na shida ya usafiri majini kwa muda mrefu, na mimi niliahidi kuwapatia kivuko wakati wa uchaguzi mwaka 2015 na ombi langu la kujenga kivuko hicho lilipokelewa vyema na serikali toka mwaka 2016 kwa ahadi ya kujenga kivuko hicho,” alisema Mabula.

Mbunge huyo alisema, kuchelewa kukamilika mapema kivuko hicho, kulitokana na changamoto kadhaa na mojawapo ni kukwama kwa vifaa bandarini kulikosababishwa na msamaha wa ushuru ambapo hata hivyo, Mabula aliahidi kushughulikia suala hilo na kufafanua kuwa Oktoba mwaka 2019 kivuko hicho kitafanyiwa majaribio rasmi kabla ya kukabidhiwa mwezi mmoja baadaye kwa ajili ya kuanza kazi rasmi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni inayotengeneza kivuko hicho ya Songoro Marine Ltd, Meja Songoro, alisema ujenzi wa kivuko hicho ulioanza Januari mwaka huu uko katika hatua za mwisho mwisho na kuwa sasa kampuni yake inakamilisha kufunga mifumo ya maji, umeme, zimamoto, kufunga ingini na vifaa vya kuendeshea kivuko hicho.