Ukaguzi vipimo wa kushtukiza wakomboa wakulima

04Jul 2020
Joseph Mwendapole
Dar es Salaam
Nipashe
Ukaguzi vipimo wa kushtukiza wakomboa wakulima

WAKALA wa Vipimo Mizani (WMA) imesema ukaguzi wa kushtukiza ambao imekuwa wakifanya nchi nzima mara kwa mara, uzimesaidia kwa kiasi kikubwa wakulima kutoibiwa na wafanyabiashara wasio waaminifu.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki Shemdoe, akitoa maagizo mbalimbali kwenye banda la Wakala wa Vipimo (WMA), kwenye maonyesho ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika Uwanja wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Kaimu Meneja Ukaguzi na Ufuatiliaji wa wakala hiyo, Almachius Pastory na Meneja wa Mawasiliano wa WMA, Irene John. PICHA: JOSEPH MWENDAPOLE

Meneja wa WMA Kitengo cha Bandari, Peter Chuwa, alisema jana kwenye Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Alisema wamekuwa wakifanya kaguzi za mizani kila baada ya miezi 12 na kukuta baadhi ya mizani imechezewa na wafanyabiashara hao kwa lengo la kuwaibia wakulima wa mazao mbalimbali kama korosho na pamba na ndiyo sababu wameamua kuwashtukiza.

Alisema WMA imesambaza namba za simu za bure ambazo wakulima na watu mbalimbali wanaohisi kupunjwa vipimo kuwapigia na maofisa wake kwenda kwa ajili ya kuwakamata wahusika na kuwachukulia hatua za kisheria kama kulipa faini.

Chuwa alisema ukaguzi wa kushtukiza wa mara kwa mara umesaidia kwa kiwango kikubwa kuwabaini wafanyabiashara wanaochezea mizani na wamekuwa wakitozwa faini kwa mujibu wa sheria.

“Hawa wafanyabiashara wakisikia WMA inaenda wanaweka mambo sawa na wala hamuwezi kukuta mzani uliochezewa lakini hizi kaguzi za kushtukiza zimesaidia sana kuwakamata na imepunguza hali ya kucheza na mizani mara kwa mara,” alisema

“Kuna watu wananamba zetu wamekuwa wakitupigia na wakati mwingine tunapata malalamiko kwa watu kupunjwa vipimo au WMA inapohisi kuna sehemu mambo hayako sawa sawa tunaenda kwa kushtukiza na kuwanasa wahusika,” alisema

Alisema wamekuwa wakienda kwenye viwanda vya nondo, tiles, maji, viwanda vya saruji kupima kama bidhaa wanazotengeneza zinawekwa vipimo sahihi kama walivyotangaza kwenye makasha yao.

“Mtu akisema hii nondo ni milimita 12 lazima tupime tujiridhishe kwamba ni milimita 12 na mfuko wa saruji unaandikwa kwamba una kilo 50 lazima tupime kama kweli ni kilo 50 na tuko makini kufanya hivyo kumlinda mlaji apate anachostahili,” alisema Chuwa.

Kaimu Meneja sehemu ya ukaguzi na ufuatiliaji, Almachius Pastory, alisema wamekuwa wakitoa elimu na kufanya kaguzi za kutosha kwenye mikoa ya Mwanza, Simiyu, Geita, Mara, Shinyanga na Kagera ili kuwalinda wakulima wa pamba wasiibiwe na wafanyabiashara wasio waaminifu.

Alisema elimu inayotolewa WMA imewezesha wakulima kujua vipimo sahihi wanapouza mazao yao na wameachana na tabia ya zamani ya kuuza mazao yao kwa kutumia vipimo batili.

“Hali hii imepunguza kwa kiwango kikubwa wanunuzi vishoka ambao wanawarubuni wakulima na wengi wamehamasika kuuza mazao yao katika vyama vya msingi na kunufaika na bei nzuri inayopangwa na serikali,” alisema

Habari Kubwa