Ukidhuru mtalii Z'bar umekwisha

24Mar 2018
Na Mwandishi Wetu
ZANZIBAR
Nipashe
Ukidhuru mtalii Z'bar umekwisha

JESHI la Polisi nchini limesema litadhibiti wahalifu wanaoibia na kudhuru watalii wanaofika Zanzibar kwa kuwa jambo ambalo linatia doa usalama uliopo katika visiwa hivyo na kuhatarisha sekta ya utalii.

Mkuu wa Operesheni Maalum za Polisi, Naibu Kamishna Liberatus Sabas

Mbali na kuendesha vita dhidi ya uhalifu kwa watalii, polisi pia imetangaza operesheni ya kukabiliana na mtandao wa dawa za kulevya visiwani hapa.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Operesheni Maalum za Polisi, Naibu Kamishna Liberatus Sabas mjini Zanzibar.

Kamanda Sabas alikuwa akiongoza timu iliyoundwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro na Kamisheni ya Polisi Zanzibar kwa lengo la kuongeza nguvu katika kuzuia na kupambana na mtandao wa dawa za kulevya pamoja na uhalifu dhidi ya watalii.

Kamanda Sabas alisema operesheni hiyo haitawaacha wahalifu hao salama kwa kuwa inafanyika kwa umakini mkubwa ili kukamata yeyote anayejihusisha na vitendo hivyo.

“Operesheni hii ni endelevu na niwape tu salamu wahalifu kuwa jambo la msingi ni wao wenyewe kujisalimisha," alisema Kamanda Sabas kwa kuwa "hata wakikimbia, tutawasaka na kuwakamata kwa kuwa nguvu ipo". 

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Kamishna Msaidizi wa Polisi Hasina Tawfiqi alisema katika operesheni hiyo wamefanikiwa kukamata dawa za kulevya aina ya heroin jumla ya kete 695 zenye ujazo wa gramu 31.3 pamoja na watuhumiwa 21.

Kamanda Mama Hasina aliwasihi wakazi wa Kaskazini Unguja na mikoa jirani kuendelea kutoa taarifa ili kuweza kukomesha mtandao wa biashara hiyo pamoja na kuhakikisha kuwa watalii wanaotembelea mkoa huo wanaondoka salama.

Operesheni hiyo pia ilifanyika katika Mkoa wa Mjini Magharibi ambako jumla ya watuhumiwa 58 walikamatwa pamoja na heroin kete 1,293 na vifuko vitatu sawa na gramu 74.385.

Habari Kubwa