Usafirishaji dhahabu ghafi mbioni kuzuiwa

04Jul 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Usafirishaji dhahabu ghafi mbioni kuzuiwa

KATIBU Mkuu Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, amesema serikali itasitisha usafirishaji wa dhahabu ghafi kwenda nje ya nchi kusafishwa baada ya viwanda vya usafishaji madini hayo kuanza kazi nchini.

Profesa Msanjila alitoa kauli hiyo jana alipofanya ziara ya kikazi katika Kiwanda cha Kusafisha Dhahabu (Refinery) cha Eyes of Africa Ltd kilichoko Area D pembezoni mwa Uwanja wa Ndege wa Dodoma.

Alisema mara baada ya viwanda vya usafishaji madini ya dhahabu kuanza kazi, serikali itasitisha usafirishaji wa dhahabu ghafi kwenda kusafishwa nje ya nchi na badala yake madini ghafi yote yatasafishiwa nchini kabla hayajasafirishwa kwenda nje ya nchi.

“Lengo la ziara hii ni kukagua hatua za ujenzi uliofikiwa na kiwanda hiki ambacho ni kiwanda cha kwanza nchini cha kusafisha madini ya dhahabu na fedha,” alisema.

Alisema kiwanda hicho ni miongoni mwa viwanda vya kampuni nne zilizopewa leseni ya usafishaji wa madini ya dhahabu (Gold Refinery Licence) nchini. Kampuni nyingine ni Stamico-Mwanza, Geita Gold Refinery na African Ayes-Geita.

Katika ukaguzi huo, Profesa Msanjila alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Eye of Africa, Ferenc Molnar, kuandika barua kwa serikali kupitia Wizara ya Madini, akiainisha mambo muhimu yanayotakiwa, ili serikali isaidie katika kufanikisha mahitaji ya kampuni hiyo.

Profesa Msanjila pia aliahidi kampuni hiyo kuwa serikali itahakikisha inapata wateja kutoka sehemu mbalimbali hususan wachimbaji wadogo mara itakapoanza uzalishaji.

Alimpongeza Molnar kwa hatua nzuri aliyoifika ikiwamo ufungwaji wa mashine mbalimbali za kusafisha madini ya dhahabu katika kiwanda hicho.

Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema kuwa mara baada ya kuanza kwa uzalishaji, kampuni yake itakuwa na uwezo wa kuzalisha kilo 40 za dhahabu kwa siku na itamtoza mteja asilimia 0.5 ya gharama ya mzigo utakaosafishwa kiwandani hapo.

Habari Kubwa