Ushirika kuuza kahawa kwa kampuni ya Japan

15Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Moshi
Nipashe
Ushirika kuuza kahawa kwa kampuni ya Japan

USHIRIKA wa vyama 32 vya ushirika wa kahawa mkoani Kilimanjaro (G32 KNCI-JVE Ltd), umetangaza kuuza kahawa yake tani 76.8 kwa kampuni ya Zensho ya Japan, kwa thamani ya Dola za Marekani 437,700.

Meneja wa ushirika huo, Gabriel Ulomi, amesema kwa sasa wako katika maandalizi ya kusafirisha kahawa hiyo kwenda nchini Japan.

Ulomi alikuwa akizungumza na Nipashe jana katika mahojiano maalum kuhusu mauzo ya kahawa na maendeleo ya mradi huo wa pamoja.

“Muda si mrefu, wakulima wataanza kunufaika na pesa za mauzo ya kahawa yao kutoka nchini Japan. Kampuni ya Zensho, licha ya kununua kahawa yetu, pia imekuwa ikitusaidia kuboresha afya za wakulima hususani afya ya mama na mtoto kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano,”alisema

Alisema Kampuni ya Zensho imekuwa na mahusiano mazuri ya muda mrefu na muungano wa vyama hivyo na kwamba mwaka huu pia wanakusudia kununua kahawa inayozalishwa bila ya kutumia dawa na mbolea za viwandani.

Zaidi ameeleza kuwa Zensho wanakusudia kununua kahawa inayozalishwa kwa njia ya kilimo hai kutoka kwa wakulima wa Mwika, Kinyamvuo na Mamba Kaskazini.

Kufuatia mafanikio hayo, Ulomi amewashauri wakulima wa kahawa mkoani Kilimanjaro kuanza kulima kilimo kisichotumia dawa wala mbolea za viwandani ili kupunguza gharama za uzalishaji la kulinda afya za wanywaji wa kahawa.

Amedai kuwa soko la kahawa linaelekea kwenye uzalishaji wa zao la kahawa isiyotumia dawa na mbolea za viwandani ili kuongeza pato la mkulima na kwamba mwaka huu kampuni ya Zensho linakuja hapa nchini kutoa elimu kwa wakulima kuhusu namna ya kuzalisha kahawa pasipo kutumia dawa na mbolea.

Alisema kampuni ya Zensho inataka kuhakikisha wakulima wanazalisha kahawa bora lakini mwaka huu, Kampuni ya Zensho tayari imetoa Dola za Marekani 33,000 kwa ajili ya kuboresha afya ya mama na mtoto.

Habari Kubwa