Utabiri sahihi hali hewa wanukia

24Mar 2018
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Utabiri sahihi hali hewa wanukia

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa jana alisema Serikali itaiwezesha Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kuwa na vifaa na mitambo ya kisasa, ili kuwezesha huduma bora za utabiri kutolewa kwa wakati na usahihi kwa manufaa ya taifa.

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa.

Prof. Mbarawa alisema hayo mjini Dodoma wakati Tanzania ikiungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa.

Waziri huyo alisisitiza kuwa kwa sasa TMA imeongeza imani kwa wananchi kwani imekuwa ikitoa utabiri wa kuaminika kwa sababu ya kuwa na vifaa vingi na vya kisasa vya utoaji taarifa.

“Nipende kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuwezesha TMA na kuhakikisha kuwa inatoa utabiri ambao ni sahihi na wa uhakika kwani kuwepo kwa utabiri sahihi kutawezesha vyombo husika kuchukua hatua mapema kabla ya madhara makubwa kutokea,” alisema.

Aidha, Waziri Mbarawa aliwataka wananchi kutunza mazingira kwa kuacha kulima kwenye vyanzo vya maji na kuepuka kuchafua maeneo ya bahari, ili kuepusha athari za uharibifu wa miundombinu ya uchukuzi.

“Niwaombe wananchi wote watunze mazingira kwani kumekuwa na uharibifu mkubwa wa miundombinu kutokana na shughuli zinazofanywa na binadamu katika maeneo mbalimbali yasiyotakiwa kulimwa au kujengwa," alisema Prof. Mbarawa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi aliishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu ya hali ya hewa, kwa kutoa fedha kununua vifaa mbalimbali ambavyo vimewezesha mamlaka hiyo kutoa utabiri ulio sahihi kwa zaidi ya asilimia 70.

Dk. Kijazi alisema kwa sasa taarifa za hali ya hewa, hasa kwenye usafiri wa anga, zimeimarika ambapo hutolewa kila baada ya nusu saa na kuwawezesha watumiaji wa usafiri huo kupata taarifa kabla ya kuanza safari zao.

“Kwa sasa utabiri wa usafiri wa anga ni wa uhakika mpaka asilimia 90... na marubani hupata taarifa hizo kwa wakati kabla ya kuanza safari zao," alisema Mama Kijazi.

Siku ya Hali ya Hewa duniani huadhimishwa kila Machi 23 ya mwaka.

Habari Kubwa