Utafiti wahimiza huduma za ugani

10Dec 2018
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
Utafiti wahimiza huduma za ugani

SERIKALI imeshauriwa kushirikisha sekta binafsi katika kuhakikisha huduma za ugani zinawafikia walengwa kwa ufanisi mkubwa na kuchochea kasi ya ukuaji wa sekta za kilimo na mifugo hapa nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bahi, ambaye pia ni Mshauri wa Utafiti, Leo Mavika, akiwasilisha taarifa ya awali ya utafiti uliofanywa na Kituo cha Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), kwa kushirikiana na Tamisemi kwenye kikao kilichowakutanisha wadau kutoka mikoa ya Njombe, Iringa, Songwe na Mbeya kilichofanyika jijini Dodoma mwishoni wa wiki. MPIGAPICHA WETU

Akiwasilisha taarifa ya awali ya utafiti uliofanywa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) na Tamisemi kwa wadau, mshauri wa utafiti huo, Leo Mavika, alisema moja ya changamoto waliyoibaini katika utafiti huo ni ushirikishwaji duni wa sekta binafsi.

“Unaweza kwenda mahali ukaambiwa kuna uhaba wa maofisa ugani, lakini kuna maofisa ugani wawili au watatu ambao wameajiriwa na asasi ya kiraia ambayo inawahudumia wakulima ambao ni wanachama wao, je, mmeshaona namna ya kuwatumia hawa kuongeza nguvu kwenye eneo unalofanya kazi?

Pia utafiti ulibainisha haja ya serikali ya kuendelea kuajiri maofisa ugani katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, ili kufikia uchumi wa kati na viwanda ifikapo mwaka 2025.

“Mwelekeo wa serikali ni kuwa kufikia uchumi wa kati ambao utaendeshwa kwa viwanda, hivyo huwezi kupuuzia sekta za kilimo, mifugo na uvuvi. Kwa hali hiyo ni lazima kuzipa nguvu kwa kuajiri wataalamu wa kutosha.

Aidha, Mavika alisema pamoja na sera kuainisha kila kata kuwa na maofisa ugani katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, hali halisi iliyobainishwa na utafiti huo ni kuwapo kwa upungufu mkubwa wa maofisa ugani katika sekta zote tatu.

Alisema pia wamebaini kuwapo utekelezaji mdogo wa sheria na viwango ambavyo vimewekwa kwenye mambo mbalimbali.

Mavika alisema pia mazingira ya ufanyaji kazi siyo rafiki kwa maofisa ugani na utoaji wa huduma za ugani.

“Hapa tumeangalia masuala yote kwa ujumla, kuanzia ofisi, usafiri na aina ya usafiri ambao unatumiwa na maofisa ugani na huduma zingine ambazo sio mazuri.

“Hali inaonyeshwa upungufu wa vyombo vya usafiri kuliko idadi ya maofisa ugani waliopo, huku vingi vikiwa ni pikipiki kuliko baiskeli.

Alisema kitu pekee kilichofurahisha ni kuwa serikali imetoa pikipiki nyingi kuliko baiskeli kwa maofisa ugani.

Mavika alisema pia imebainika kuwa uelewa wa wataalamu kwenye maeneo mbalimbali ikiwamo hata eneo la kitaalumu ni mdogo kwa baadhi ya watu.

Alisema pia wamebaini kuwapo kwa shida ya uratibu kuanzia ngazi ya wizara, mikoa hadi serikali za mitaa hususan kwenye upangaji wa kazi, utekelezaji, ufuatiliaji, tathmini na uhusiano na wadau.

Habari Kubwa