Utashi kisera, kisiasa waelezwa chachu katika usimamizi misitu

24Nov 2022
Christina Haule
DODOMA
Nipashe
Utashi kisera, kisiasa waelezwa chachu katika usimamizi misitu

UTASHI wa kisera na kisiasa umeelezwa kuwa ni jambo la msingi kwa viongozi kuamua kuwashirikisha wananchi katika utekelezaji wa usimamizi shirikishi wa misitu (USMJ) ili kuona tija ya uhifadhi na kunusuru uharibifu wa misitu.

Mwakilishi wa Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania, Clara Melchior, alisema hayo jana kwenye mkutano wa wadau wa misitu na serikali katika kuangalia namna ya kuwekeza kifedha katika usimamizi wa misitu kilichofanyika jijini hapo.

Alisema mradi wa kuhifadhi misitu kwa kuwezesha biashara endelevu ya mazao ya misitu Tanzania (CoForEST) unaotekelezwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) kwa kushirikiana na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo na Ushirikiano Uswisi (SDC) ni muhimu ukapewa nguvu zaidi kisera na kisheria kupitia wanasiasa na viongozi.

Kwa kufanya hivyo, alisema mradi huo utaendelea kuzaa matunda kwa wanavijiji kuwa na moyo wa kusimamia misitu baada ya kuona faida ya utunzaji.

Melchior alisema kupitia utafiti walioufanya kupitia wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), wamebaini bado kuna mahitaji ya kuendelea na hatua ya tatu ya mradi huo ambao unamalizika mwezi ujao baada ya kutambua kuwa kuna umuhimu wa kupanua wigo wa ushirikishaji wanavijiji kusimamia rasilimali za misitu ya vijiji (USMJ).

Alisema upanuzi wa wigo huo unapaswa kwenda sambamba na kuwajengea uwezo wadau wakubwa wa misitu wakiwamo serikali kuu na za vijiji ambao ndio wenye nguvu kisera na kisheria pamoja na asasi za kiraia ili waone utaratibu mzima wa mradi unavyotekelezwa na kubaini maana ya mradi na kuuendeleza hata pale mradi utakapofikia mwisho.

Akifungua mkutano huo, Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Deusdedit Boyo, alisema serikali ina mpango wa kusimamia halmashauri zote nchini kutenga fedha katika bajeti za kila mwaka kwa ajli ya kuangalia misitu sambamba na kutumika katika usimamizi na uhifadhi wa misitu.

Boyo alisema utengaji fedha hizo, unapaswa kwenda sambamba na kuzijengea uwezo halmashauri kwa sababu kuna baadhi ya watu hawafahamu umuhimu wa misitu katika mazingira ya kawaida na kuingia kukata kuni na kufanya shughuli zingine za uharibifu wa misitu.

Alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na misitu hekta milioni 48.1 yakiwamo maeneo  makubwa yanayoanguka katika ardhi za vijiji yakiwa na hekta milioni 22 na kati ya hekta hizo ni chache ambazo zimeshakidhi kuingia katika mpango wa usimamizi shirikishi.

Kwa mujibu wa Bayo, serikali kupitia wizara hiyo, iko katika mkakati wa kuhakikisha misitu mingi inahifadhiwa kwa sababu inapokuwa haijahifadhiwa kisheria inaweza kuharibiwa.

Alisema tayari wameshatekeleza mkakati wa Sera ya Taifa ya Misitu ambao ndio dira ya kuendeleza misitu katika kipindi cha miaka 10 ijayo kuanzia mwaka 2021 hadi 2031. Pia alisema wametengeneza mpango kazi wa usimamizi shirikishi wa misitu hasa katika vijiji kwa lengo la misitu mingi kuwa katika hifadhi za vijiji na kuhifadhiwa kisheria.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TFCG, Charles Meshack, alisema mradi wa CoForEST una uwezo wa kulinda na kuhifadhi mazingira na kwamba suala la kutoweka kwa misitu nchini linasababishwa na watu wanaofanya shughuli za mbalimbali kwenye ardhi ikiwamo kilimo, mkaa na ulishaji mifugo.