Utii sheria waokoa vyanzo vya maji

06Jan 2019
Stephen Chidiye
Tunduru
Nipashe Jumapili
Utii sheria waokoa vyanzo vya maji

UTEKELEZAJI wa sheria ndogo za mazingira katika baadhi ya vijiji vilivyoko Tunduru mkoani Ruvuma, umesaidia kuokoa vyanzo vya maji na kuendelea kuwapo uhakika wa upatikanaji wa huduma hiyo.

CHANZO CHA MAJI

Hayo yalibainishwa na wanachama wa jumuiya za watumia maji katika bonde dogo la Mto Msinjewe, Saidi Kamwana, wakati wa  mafunzo ya kujengewa uwezo wa namna ya kutunza na kuhifadhi mazingira na  vyanzo vya maji yaliyofanyika katika ukumbi wa klasta ya walimu wa Tarafa ya Mlingoti mjini hapa.

 

Akitoa ushuhuda wa mafanikio ya utekelezaji wa sheria hizo, Kamwana ambaye ni Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Msingili, alisema katika utekelezaji huo,  wananchi sita walikamatwa katika kipindi cha mwaka jana na kuhukumiwa faini ya Sh. 20,000/= kila mmoja baada ya kukamatwa wakivunja sheria hiyo.

Kamwana alisema katika utekelezaji huo, wananchi hao walikubaliana kutolima wala kukata miti katika maeneo yote yaliyomo katika vyanzo vya maji ili kulinda uoto wa asili na kujihakikishia upatikanaji wa maji wakati wote na kwamba atakayekiuka maelekezo hayo, atatozwa faini hiyo na akishindwa kulipa atashtakiwa katika baraza la kata.

 

Awali, Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Bonde la Ruvuma na Pwani ya Kusini, Dikson Maganga, alisema mafunzo hayo yanatolewa ili kuwajengea uwezo wa kutambua na kujiwekea mikakati ya matumizi wakati wakifanya shughuli za kibinadamu katika mito na mabwawa ya maji.

 

Maganga alisema hali hiyo imetokana na idara yake kubaini kuwapo kundi la watu wengi ambao wamekuwa wakikiuka sheria na kufanya shughuli zao ndani ya mita 60 na kwamba kwa kufanya hivyo, wanahatarisha uhai wa vyanzo vya maji na kuliweka taifa katika hatari ya ukame.

 

Naye mkufunzi wa mafunzo hayo, Regnald Mapunda, pamoja na kuwataka wanajumuiya hao kujikita katika sera na sheria ya maji, alisema shughuli nyingi za kibinabamu zimekuwa zikifanyika holela, hivyo ni muhimu kuwekwa taratibu za kudhibiti vitendo hivyo.

 

Mapunda alisema tabia za wananchi wengi kuruhusu mifugo kuzurura katika maeneo ya vyanzo vya ni janga lingine ambalo endapo utaratibu huo hautadhibitiwa na kuachiwa uendelee, kuna hatari ya kulipeleka taifa katika vita ya tatu ya dunia ambayo itahusisha binadamu kugombea maji miaka michache ijayo

Habari Kubwa