Utouh ataka uwazi ripoti za CAG

24May 2019
Paul Mabeja
DODOMA
Nipashe
Utouh ataka uwazi ripoti za CAG

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Ludovick Utouh, amesema ripoti za ukaguzi zinazofanywa na Ofisi ya CAG zinapaswa kuwa taarifa za wazi kwa umma.

CAG huyo mstaafu alitoa kauli hiyo juzi katika mapitio ya ripoti ya CAG kwa mwaka 2017/2018 kwa wakurugenzi wa mtandao wa asasi za kiraia nchini wa kanda ya kati, katika kikao kilichofanyika jijini hapa.

Alisema ripoti hizo zinaonyesha mapato na matumizi ya fedha za bajeti zilizopitishwa na bunge ambazo kwa kiasi kikubwa zinatokana na walipa kodi, hivyo zinatakiwa kuwa wazi.

Utouh ambaye pia Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wajibu, alisema ripoti hizo ndilo jicho la Watanzania kwenye usimamizi wa rasilimali zao kwa kuwa ndizo pekee zinazochanganua mapato na matumizi ya bajeti na utekelezaji wake.

Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa Asasi za Kiraia Mkoa wa Dodoma, Sarah Mwaga, alisema ripoti hizo zinapaswa kutolewa katika mfumo na lugha rahisi itakayowafikia wananchi wengi ili kuwajengea uelewa na kuhoji mambo mbalimbali yanayohusu maendeleo yao hasa kutoka serikali kuu na serikali za mitaa.

Washiriki wa kikao hicho, Askofu Amon Kinyunyu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Dodoma na Sheikh Rashid Bura kutoka taasisi ya Kiislamu ya Dalai, walisema ofisi hiyo ndiyo muhimili wa shughuli za maendeleo na kuomba iwe huru bila kuingiliwa na mihimili mingine.

Naye Ofisa Mfawidhi Kitengo cha Kujengwa Uwezo wa Asasi kutoka Foundation for Civil Society (FCS), Nasim Losai, alisema warsha hiyo inakutanisha wakurugenzi ili kuzungumza na kutoa na fikra mbadala.

Vile vile alisema kuwa kuna ulazima kwa asasi za kiraia kuwa makini kutokana na suala la maombi ya ruzuku kuhusishwa na masuala ya rushwa.

Habari Kubwa