Utumaji barua kwa Posta waongezeka

05Jul 2019
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Utumaji barua kwa Posta waongezeka

UTUMAJI wa barua kwa njia ya Posta umeongezeka kutoka asilimia 26 ya mwaka 2016/17 hadi kufikia asilimia 36 kwa mwaka 2018/19.

Pia mauzo ya stempu kwa mwaka 2017/18 yamepanda kwa asilimia 36 ukilinganisha na kiwango kidogo kilichouzwa mwaka 2016 ilipoanzishwa.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika Maonyesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa Kaimu Meneja wa Barua na Usafirishaji wa shirika hilo, Hadija Iddi, alisema ongezeko la kutuma barua limetokana na uwapo wa barua za ndani ambazo ni za kuomba kazi, nyaraka za shuleni na nyaraka za maofisini.

Alisema biashara hizo za stempu za kumbukumbu zimekuwa zikifanywa zaidi na nchi za nje zikiwamo China, Marekani, Canada, Uingereza, Indonesia, Italia, India na Autralia.

Alisema barua za nje mwaka 2016/17 zilishuka kwa asilimia 50, lakini mwaka 2017/18 zikapanda kwa asilimia 37.

Alisema matumizi ya mtandao, hayajaathiri utumaji barua, kwa sababu kuna nyaraka ambazo bado zinahitaji kutumwa kwa njia ya Posta na shirika lao linaaminika.

Akizungumzia mauzo ya stempu, Iddi alisema watu wanatumia stempu kama kumbukumbu kwa ajili ya vivutio vya utalii, wanyama, picha za watu mashuhuri yalipanda kwa asilimia saba mwaka 2017/18.

Alisema biashara hiyo ya stempu za kumbukumbu imekuwa kwa sababu ya kuanzisha kwa huduma ya stempu mtandao.

Pia alisema shirika lao linatoa huduma ya kusafirisha mizigo ikiwamo kuhamisha vifaa vya ofisini na majumbani kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine.