Uuzaji hisa DSE sasa kwa simu

21Nov 2020
Beatrice Moses
Dar es Salaam
Nipashe
Uuzaji hisa DSE sasa kwa simu

SOKO la Hisa la Dar es Salaam (DSE), linatarajiwa kuongeza idadi ya wanahisa baada ya kuzindua mfumo mpya wa uuzaji hisa, kupitia simu za mkononi.

Mfumo huo unaotajwa kwa jina la ‘Hisa Kiganjani’ ulizinduliwa jana jijini Dar es Salaam, unatarajiwa kuongeza idadi ya wawekezaji 550,000 waliopo sasa.

Akizungumza jana kuhusu mfumo huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Moremi Marwa, alisema mfumo huo utarahisisha wawekezaji kujiunga na kununua hisa bila kuhudhuria kwenye eneo la soko.

“Mfumo huo unatoa nafasi wa DSE kujitanua kutoka Dar es Salaam kufika kwenye maeneo mengine ya nchi kupitia simu ya mkononi, tunaamini itatoa fursa kwa watu wengi wafanyabiashara na wajasiriamali  kujiunga, hivyo kujiongezea kipato,” alisema Marwa.
 
Alisema kufanikiwa kuanza kutumika kwa mfumo huo kumehusisha taasisi kadhaa ikiwamo, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Mfumo wa Malipo ya Kielektroniki Serikalini (GePG).

Akizindua mfumo huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Nicodemus Mkama, alisema uwapo wa mfumo huo unatarajiwa kuleta matokeo chanya katika kujenga sekta jumuishi ya fedha.
 
Alisema mfumo huo unaweza kuwavutia wananchi wanaotumia simu za mkononi ambao  kwa takwimu zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kipindi kilichoishia Septemba mwaka huu, Watanzania milioni 49.2  wanatumia simu, kati yao milioni 30.5 wanatumia huduma za fedha kwa njia ya  simu.

“Mfumo huo unatarajia kuwezesha kuongezeka kwa miamala katika soko la hisa, inatarajiwa ukwasi wa soko la hisa utaongezeka, ni kiashiria muhimu cha ubora wa soko kinachovutia wawekezaji wengi wa ndani na wa kimataifa,” alisema Mkama.

Alisema mfumo huo umeidhinishwa baada ya CMSA kujiridhisha kuwa unakidhi matakwa ya sheria, ni salama kwa wawekezaji.

Mkama alisema CMSA itaendelea kujenga mazingira wezeshi na shirikishi kwa lengo la kuhakikisha maendeleo ya masoko ya mitaji yatapatikana, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.  
 

Habari Kubwa