Uwekezaji wa kisima cha mafuta wawagonganisha wananchi, DC

22Mar 2016
Gideon Mwakanosya
Songea
Nipashe
Uwekezaji wa kisima cha mafuta wawagonganisha wananchi, DC

BAADHI ya wananchi wa kijiji cha Kilosa Juu Wilaya Nyasa mkoani Ruvuma, wamemlalamikia Mkuu wa wilaya hiyo, Magreth Malenga, kwa kutumia amri ya kuwataka wahame katika maeneo yao wanayoishi kabla ya kulipwa fidia zao.

Mkuu wa wilaya kilosa, Magreth Malenga.

Wananchi hao wanatakiwa kuhama kwenye maeneo hayo ili wampishe mwekezaji anayetaka kutumia sehemu ya eneo la kijiji hicho kujenga kituo cha kuuza mafuta.

Aidha, walisema wameshangazwa na kitendo hicho wakidai kuwa anatumia nguvu kutaka wananchi hao waondoke, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na taratibu za nchi.

Kwa msingi huo, wameiomba serikali kuingilia kati ili wapate haki yao ya msingi.

Walisema wasipopewa malipo ya fidia zao ipasavyo, hawatahama mpaka utakapofanyika upembuzi yakinifu juu ya malipo hayo katika maeneo wanayoishi.

Kadhalika walieleza kwamba kumekuwa na usiri mkubwa uliogubikwa juu ya mwekezaji huyo ambapo Machi 9, mwaka huu, ulifanyika mkutano kijijini hapo na Mkuu huyo wa Wilaya na walipomtaka aeleze bayana juu ya nani anayetaka kuwekeza katika eneo hilo, hakumtaja.

“Huyu Mkuu wa wilaya anatushangaza sana, tulipofanya mkutano wa kijiji wananchi waliuliza maswali ya kumtaka hili jambo lisiwe linafanyika kwa usiri, watu walipohoji na kumtaka atuambie ni nani anayetaka kuja kujenga kituo hiki cha kuuzia mafuta, alikataa kumtaja," alidai Said Hussein, mkazi wa kijiji hicho.

Kwa upande wake, Ester Mahepano, alisema watu walipokuwa wakihoji kutaka kujua ukweli na uwazi juu ya jambo hilo, Mkuu wa Wilaya alikuwa akiwajia juu na kuwaamuru wakae chini.

"Tulimuona Mkuu wa Wilaya akiwa na maofisa wa ardhi wakizunguka katika maeneo yetu na kupima ardhi. Tangu ameanza mchakato huu, hajatushirikisha wananchi ipasavyo, haya mambo anayafanya peke yake akiwa na viongozi wenzake wa halmashauri,” alidai Yakobo Komba.

Akijibu malalamiko ya wananchi hao, Mkuu wa wilaya hiyo, Malenga alisema eneo hilo katika mchoro wake limetengwa kwa ajili ya uwekezaji wa aina mbalimbali.

Alisema hivyo wananchi wanapaswa kulielewa hilo na kwamba yeye kama Mkuu wa Wilaya ataendelea kulisimamia hilo.

Hata hivyo, aliwaasa wananchi wenye maeneo hayo, kupeleka malalamiko yao ofisini kwake pale itakapoonekana wamepunjwa malipo yao ya fidia na kumtaka Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, kulipatia suala hilo umuhimu wa kipekee.

Diwani wa kata ya Kilosa, Stanley Vumu, alithibitisha kuwapo kwa malalamiko hayo ya wananchi akidai kuwa tayari hatua husika zimeanza kuchukuliwa kwa lengo la kumaliza mgogoro huo.

“Hii shughuli ya kupima yale maeneo tumesitisha kwanza, tutaendelea na mchakato siku zijazo baada ya wananchi watakapokuwa wameelimishwa na kuelewa juu ya umuhimu wa kujenga kituo hiki cha mafuta,katika wilaya yetu,” alisema Vumu.

Vumu aliongeza kuwa ni vema serikali kupitia watendaji wake wakaliweka sawa suala hilo ili wananchi wapate haki zao huku akiwataka wananchi nao kuwa watulivu wakati yeye akiendelea na jitihada za kuwasiliana na mamlaka husika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, Jabir Shekimweri alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, alisema wanatarajia kupima eneo lenye ukubwa wa ekari moja na nusu na kwamba nyumba takriban nane katika eneo hilo zitvunjwa.

Habari Kubwa