Uzalishaji mbegu bora mkonge kuongezeka

22Jan 2021
Ashton Balaigwa
Tanga
Nipashe
Uzalishaji mbegu bora mkonge kuongezeka

TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), inakusudia kuzalisha mbegu bora ya mkonge  kutoka miche milioni 2.5 ya sasa inayozalishwa kwa njia ya vikonyo kufikia milioni 10 kwa mwaka itakayozalishwa kwa njia ya chupa.

Hatua hiyo ni baada ya kuifanyia ukarabati maabara yao iliyopo katika Kituo cha TARI Mlingano mkoani Tanga.

Uzalishaji huo unalenga kukidhi mahitaji ya soko la  dunia la mkonge taklibani tani 500,000 kwa mwaka wakati uzalishaji kwa sasa ni tani 280,000, huku  Tanzania ikiwa ya pili kwa uzalishaji huo ikizalisha wastani wa tani 40,000 kiasi ambacho ni kidogo ukilinganisha na fursa iliyopo ya uzalishaji.

Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk. Geofrey Mkamilo, alisema uzalishaji wa mbegu bora za mkonge unafanywa kwa kutumia vikonyo ambao unazalisha miche milioni 2.5 kwa mwaka hivyo maabara ya Tissue Culture itakapofanyiwa ukarabati wa kina itaongeza na kufikia milioni 10, hivyo kukidhi mahitaji ya mbegu wa wakulima wa mikoa yote inayolima mkonge.

“Tunataka kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora, na hapa tunapozungumza tumeshapanda shamba lenye hekta 31.2 ambapo kuna miche taklibani 2.5 lakini tunataka kuongeza, uzalishaji kwa kutumia maabara baada ya kuifanyia ukarabati mkubwa.

Alisema maabara hiyo inazalisha miche bora taklibani 120,000, lakini ikipanuliwa itaongeza upatikanaji wa mbegu na kufikia miche milioni 10 kwa njia ya chupa  kwa mwaka.

Dk. Mkamilo alisema mahitaji ya sasa ya mbegu ya mkonge kwa wakulima wadogo ni miche kati ya milioni 1.2 hadi milioni 1.6, huku wakulima wakubwa wakihitaji miche kati ya milioni 10 mpaka milioni 12.

Alisema kuwa Tanzania ina eneo la hekta 44,123,561 sawa na asilimia 47 linalofaa kwa kilimo cha mkonge wakati eneo linalolimwa ni hekta 64,029.73 sawa na asilimia 0.2 hivyo endapo uzalishaji wa mbegu kwa kutumia maabara utafanikiwa, utasaidia kuongeza uzalishaji wa mkonge.

Mwenyekiti wa Bodi ya TARI, Dk. Yohana Budeba, akizungumzia kuhusu kilimo cha mkonge , alisema walitoa muongozo wa TARI Mlingano kuzalisha mbegu bora za kisasa ili kutekeleza agizo la Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa, la kufufua upya zao hilo kwa kuhakikisha mbegu zinazalishwa kwa wingi.

Awali Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Mlingano kilichopo Mkoani Tanga, Dk Catherine Senkoro, alisema kituo kimepewa jukumu la kitaifa la kutafiti na kuendeleza zao la mkonge na utafiti wa rasilimali ardhi ya kilimo ikiwamo afya ya udongo ,maji na matumizi sahihi ya mbolea pamoja na kuhakikisha teknolojia zinawafikia wakulima kwa wakati.

Habari Kubwa