Uzalishaji wa kuku kuongezeka nchini

04Jul 2020
Ibrahim Joseph
Dodoma
Nipashe
Uzalishaji wa kuku kuongezeka nchini

SERIKALI imejipanga kuongeza uzalishaji wa kuku kupitia vikundi vya vijana, ili kujikwamua kiuchumi na kukidhi mahitaji ya soko nchini.

Mkurungenzi wa Uzalishaji na Masoko wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Felix Nandonde, alibainisha hayo alipokabidhi vifaranga vya kuku 650 wa nyama kwa kikundi cha vijana cha Asacri cha jijini.

Dk. Nandonde alisema wizara imeendelea na utaratibu wa kukabidhi misaada ya vifaranga vya kuku kwa makundi ya vijana, ili kuwakwamua kiuchumi na kutoa ajira kwao.

Alibainisha kuwa msaada huo ni miongoni mwa mikakati ya wizara hiyo ya kuyahamasisha makundi mbalimbali ya kijamii kupenda ufugaji wa kuku.

“Leo tumekabidhi vifaranga vyenye thamani ya Sh. milioni tatu na tunatarajia kuongeza kadri ya bajeti ya wizara itakavyoruhusu, ili kuzalisha kuku wengi kukidhi soko la wakazi wa Jiji la Dodoma,”alisema.

Alisema wizara hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Akm, wametoa idadi hiyo ya vifaranga wa nyama, ili kuongeza nguvu katika ufugaji wa kuku nchini.

Alisema mbali na msaada huo, wamekabidhi vifaa, chakula na dawa kwa ajili kuwahudumia kuku hao na uongozi wa jiji utatoa  madaktari kwa ajili ya kuwapa mafunzo namna ya kuwahudumia kuku hao.

Alisema mpaka sasa, kuna kuku milioni 79.1 nchini. Kati yao, wa kienyeji ni milioni 38.5 na wa kisasa milioni 40.6.

Aliongeza kuwa mpango huo wa kuyawezesha makundi ya vijana utakuwa endelevu na unafanyika kwa awamu katika mikoa mbalimbali nchini.

Kijana Abdalah Chavuma kutoka Kikundi cha Asacri, alisema kikundi chao kinaundwa na vijana 10 wa jinsia tofauti ambao ni wahitimu wa vyuo vikuu mbalimbali nchini.

Chavuma alisema kikundi chao kinajihusisha na ufugaji wa kuku, sungura na bata na wako katika maeneo ya Nkuhungu na Chidachi jijini hapa.

Meya wa Jiji la Dodoma, Profesa David Mwamfupe, alisema moja ya malengo ya jiji hilo ni kuhakikisha wanayawezesha makundi mbalimbali ya kiuchumi.

Profesa Mwamfupe alisema mbali na uongozi wa jiji kutoa fedha kwa ajili ya makundi hayo, pia wanawezeshwa mikopo ya ng’ombe wa maziwa, ili kujiajiri na kuajiri wengine.

Profesa Mwamfupe aliyataka makundi hayo ya vijana kuchangamkia fursa za ajira zinazojitokeza katika maeneo yao.

Habari Kubwa