Veta yawafunda mama, babalishe

09Jan 2017
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Veta yawafunda mama, babalishe

MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) Kanda ya Kaskazini imetoa mafunzo kwa sekta isiyo rasmi yanayolenga kuboresha shughuli zao na kuongeza wigo wa ajira.

Mafunzo hayo ni muendelezo wa programu ya utaoji mafunzo kwa sekta isiyo rasmi iliyoanzishwa zaidi ya miaka 10 iliyopita, ambayo inalenga makundi yanayoendesha shughuli za kiuchumi sehemu mbalimbali Tanzania.

Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa kufunga mafunzo ya siku sita kwa mamalishe na babalishe 69 wanaozunguka soko la Kilombero, mtafiti wa soko la ajira kutoka Veta, John Tesha, alisema programu hiyo ni ya kwanza kuendeshwa jijini Arusha.

Alisema mama lishe na baba lishe hao wamepatiwa mafunzo ya ujasiriamali na kuanzisha biashara na kujua njia bora za upikaji kwa kuzingatia sheria na kanuni za usafi.

Alisema lengo la kutoa mafunzo hayo ni kuwatoa walengwa kwenye sekta isiyo rasmi na kuwaingiza kwenye sekta rasmi ili waweze kuongeza wigo wa ajira na kupata kipato cha uhakika.

"Programu hii inalenga Watanzania wanaofanya shughuli zao katika sekta isiyo rasmi kama mama lishe, ufugaji wa kuku wa asili, nyuki, kilimo na ufugaji bora pamoja na sekta tofauti kulingana na mahitaji yao, " alisema.

Kwa upande wa mama lishe na baba lishe waliopata mafunzo hayo, walisema wamefurahishwa na mafunzo hayo kwani yamewawezesha kujua mambo mengi ambayo yatawasaidia kuboresha biashara zao na kupika kwa usafi zaidi.

Hata hivyo, mmoja wa mamalishe kutoka soko la Kilombero, Flora Kileo, alisema wanaiomba serikali iwaboreshee mazingira ya soko hilo kwani lipo katika hali ya uchafu ambayo inachangia kutopata wateja wengi, huku pia wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama.

Alisema mazingira ya soko hilo kuwa kwenye mazingira magumu kunachangia chakula kuuzwa kwa bei rahisi ili kupata wateja na hivyo kusababisha wapate faida kidogo pamoja na chakula kuwa kizuri.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Levolosi, Esther Maganza, aliwataka mamalishe na babalishe hao kutumia vizuri maarifa waliyoyapata ili wawe na wigo mpana wa kiuchumi wa kuwasaidia kipato katika familia zao na vikundi walivyonavyo.

Aliwataka kuwatumia maofisa ushirika na maendeleo ya jamii wa kata ambao wana ujuzi wa kuwapatia mwongozo wa namna ya kuanzisha vikundi vya ushirika ili kuongeza nguvu ya kuleta maendeleo .

Habari Kubwa