Vibali uagizaji dawa vyaongezeka

17Jan 2020
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Vibali uagizaji dawa vyaongezeka

MAMLAKA ya Chakula na Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), imeongeza idadi ya vibali vya uingizaji na utoaji wa bidhaa nje ya nchi kutoka vibali 13,018 kwa mwaka 2015/16 hadi vibali 26,478 mwaka 2018/19, sawa na ongezeko la asilimia 203.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo, picha mtandao

Imeelezwa kuwa mafanikio hayo yametokana na kuwapo kwa mfumo wa kielektroniki wa utoaji vibali vya kuingiza na kutoa bidhaa nchini, unaowezesha wateja kutuma maombi na kufanya malipo popote walipo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo, aliyasema hayo katika ofisi za mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na maofisa mawasiliano kutoka katika taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto katika ziara ya kampeni yao ya 'Tumeboresha Sekta ya Afya'.

"Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa serikali ya awamu ya tano, TMDA ambayo awali ilikuwa TFDA, tumefanikiwa kuboresha huduma hasa za utoaji wa vibali baada ya kuwa na mfumo huu mpya unaotoa huduma kisasa," alisifu.

Alisema mamlaka hiyo pia imefanikiwa kupunguza idadi ya bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba visivyofaa kwa matumizi ya binadamu, baada ya kuboresha utendaji kazi, kutoka tani 140,705 mwaka 2017/18 zilizokuwa na thamani ya Sh. milioni 22.394 hadi kufika tani 664 mwaka 2018/19.

"Hii inaashiria kupungua kwa bidhaa zisizokidhi viwango katika soko la Tanzania kutokana na kazi kubwa inayofanywa na mamlaka za kudhibiti uaingizaji," alifafanua.

Alisema wanadhibiti, kuondoa na kuteketeza bidhaa ambazo hazikidhi vigezo vya ubora, usalama na ufanisi ili kuepusha zisitumiwe na walaji.

Alisema kufuatia mpango wa ufuatiliaji wa ubora wa bidhaa katika soko, sampuli 1,136 za dawa za binadamu zilifuatiliwa na kuchunguzwa katika kipindi cha miaka minne na asilimia 96 ziliendelea kukidhi vigezo vya ubora.

Alieleza kuwa kati ya sampuli 144 za dawa za mifugo zilizochunguzwa katika kipindi hicho, asilimia 90 zinaendelea kukidhi vigezo vya ubora.

Fimbo alisema mamlaka pia imeweka mifumo madhubuti ya ufuatiliaji wa madhara yatokanayo na matumizi ya dawa na vifaa tiba ili kutambua, kutathmini na kuzuia madhara yasiyovumilika yasitokee kwa wananchi.

Alisema ili kuimarisha upatikanaji wa taarifa hizo, TMDA imeanzisha mfumo wa kielektroniki wa utoaji wa taarifa za madhara yatokanayo na matumizi ya dawa kwa kutumia simu ya mkononi au kompyuta na njia ya kutuma ujumbe wa simu.

Kuhusu mipango na malengo ya TMDA, alisema wanalenga kujenga maabara kubwa na ya kisasa ofisi za makao makuu za jijini Dar es Salaam na Dodoma ili kuboresha utendaji kazi wa mamlaka hiyo.

Alisema jengo lake litakuwa la ghorofa saba likiwa na maabara kubwa na ya kisasa, vifaa tiba, vitendanishi na vifaa vya kutosha.

Habari Kubwa