Vibali vya uagizaji mbolea vyafutwa

30Jul 2021
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
Vibali vya uagizaji mbolea vyafutwa

​​​​​​​WIZARA ya Kilimo imefuta utoaji zabuni na vibali vya uagizaji mbolea nchini ili kutoa nafasi kwa wafanyabiashara kuleta mbolea kwa wingi na kwa gharama nafuu.

Hata hivyo imechukua mikakati mbalimbali ya kushuka bei ya mbolea za kupandia na kukuzia.

Waziri wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda, alisema wameamua kufanya hivyo ili kutoa nafasi kwa wafanyabiashara au mtu yeyote kuagiza mbolea hiyo kwa wingi lakini kwa sharti la kukaguliwa na Mamlaka ya kudhibiti mbolea nchini ili ziwe na ubora unaotakiwa.

Alisema ufutaji wa zabuni na kupunguza mlolongo wa utoaji vibali vya kuagiza mbolea utasaidia kuongeza ushindani wa kuleta mbolea hapa nchini na hivyo kupunguza gharama.

“Sasa hivi mtu yeyote anayeweza kuleta mbolea nchini alete mradi tu ubora wa mbolea uwe umehakikiwa na kibali cha kuingiza mbolea kinatolewa na mamlaka yetu ya kudhibiti ubora wa mbolea sio kwamba lazima uwe kwenye orodha,” alisema.

Alitaja mkakati mwingine kuwa ni kupunguza muda wa shehena ya mbolea kukaa muda mrefu bandarini.

“Mkakati wa tatu ni pamoja na kuleta mbolea nyingi kwa wakati mmoja na kama kuna uwezekano wa kuuza nje wauze kwa sababu unaponunua mzigo mkubwa bei inakuwa na uafadhali zaidi kuliko ukileta mzigo mdogo,” alisema.

Akizungumzia kuhusu mazungumzo yake na kampuni ya Mbolea ya Taifa (OCP) ya Morocco ambayo inaleta mbolea aina ya ACP na ACP Zink, Waziri huyo alisema mazungumzo hayo yamefika mahali pazuri na wamekubaliana kuwa mbolea hizo zitauzwa kwa Sh. 60,000 kwa mfuko wa kilogramu 50 na Zink ACP itakuwa ikiuzwa kwa Sh. 65,000.

Alisema mbolea hiyo ni bora kama ilivyo mbolea ya DAP ambayo wakulima wamezoea kuitumia katika kupandia mazao na kuoteshea na kuongeza kuwa mbolea hiyo inauzwa kwa Sh. 75,000 kwa jijini Dar es Salaam na ikifika mikoani itapanda kidogo.

Alisema OCP wanaingiza mbolea aina ya CAN na mbolea hiyo itauzwa kwa Dar es Salaam mfuko wa kilogramu 50 na itauzwa kwa Sh. 48,000 wakati mwaka jana mfuko huo ulikuwa unauzwa Sh. 46,000 na kuna nyongeza kidogo imetokea lakini si kubwa sana kutokana na mfumuko wa bei ya mbolea ulivyokuwa mkubwa duniani.

“Shehena iliyopo hapa nchini itaendelea kuuzwa kwa bei hiyo hiyo ya mwaka jana mpaka pale itakapoisha, lakini bado kwenye meli kuna nyingine zinaendelea kuwasili kwa ajili ya kuleta mbolea ndani ya mwezi huu na ujao lakini wafanyabiashara wanazidi kuomba vibali vya kuleta bidhaa hii,” alisema.

Kuhusu soko la mahindi, alisema wamepata nchiniSudan Kusini kwa ajili ya kupeleka tani 200,000 za nafaka, huku tani 144,000 kwa ajili ya soko la mahindi Mombasa.

Pamoja na hatua hiyo, alisema pia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imekabidhiwa Sh. bilioni saba kwa ajili ya kuagiza chakula na bodi ya mazao mchanganyiko wamepewa Sh. bilioni tano kwa ajili ya kununua bidhaa.

Mwakilishi wa Kampuni ya OCP Tanzania, Dk. Mshindo Msola, alisema kampuni hiyo ilianza kufanya kazi mwaka 2017 baada ya Mfalme wa Morocco kufika nchini kwa ziara ya kikazi na tangu kipindi hiko wamekuwa wadau wakubwa wa kilimo nchini kwa kutoa mbolea zenye ubora wa hali ya juu na kwa bei rahisi.

Habari Kubwa