Vijana 28,000 wanolewa ujasiriamali

15May 2019
Allan lsack
ARUSHA
Nipashe
Vijana 28,000 wanolewa ujasiriamali

TAASISI isiyokuwa ya kiserikali ya Arusha Municipal Community (AMCF), kwa kushirikiana na Shirika la Foundation for Civil Society (FCS), kupitia mradi wa majukwaa ya vijana, wametoa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana 28,000,-

wa kata tatu za Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa lengo la kuwakomboa na wimbi la umasikini.

Akizungumza wakati wa mashindano ya maonyesho ya bidhaa kutoka kwa vijana hao, Ofisa Tawala Msaidizi wa Shirika la AMCF, Anna Mushi, alisema mafunzo hayo, walitoa kupitia majukwaa ya vijana wa Kata za Lemara, Unga limited na Sokoni One, lengo likiwa kuwasaidia vijana kiuchumi kwa kuwafundisha njia za uhakika za kuzalisha bidhaa bora ili waweze kujiajiri.

Alisema, kupitia mradi huo, wamekuwa wakiwakusanya vijana kwa pamoja katika kata hizo, kwa ajili ya kutoa mafunzo ya uongozi, utawala bora, mafunzo ya kushiriki katika shughuli za kiserikali kwa ajili ya maendeleo, kutambua fursa zilizopo kwenye jamii na kushiriki katika ngazi za kutoa maamuzi.

Aliongeza kuwa kupitia mradi huo, wamefanikiwa kutoa elimu kwa vijana ya ujasiriamali na masoko, biashara na ubunifu ili waweze kukuza na kuongeza vipato vyao vya kiuchumi.

"Tunawahamasisha vijana nchini kuwa wajasiriamali wasitegemee kuajiriwa waliopo vyuoni, tuanze kufikiria hili ili serikali inapofanya kampeni ya kuwa na nchi ya viwanda tunawashauri kujiunga katika makundi mbalimbali kwa ajili ya kuanzisha viwanda vidogo ambavyo vitaifanya nchi uchumi wake kukua kwa kasi," alisema Anna.

Ofisa Idara ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Jiji la Arusha, Hanifa Ramadhani, alisema katika bajeti ya mwaka 2018/19, halmashauri hiyo, ilitoa mikopo ya Sh. milioni 665 kwa vikundi 118, kutoka kata 25 za Jiji la Arusha.

Alisema maelekezo ya serikali mwaka wa bajeti kila halmashauri inatakiwa kutenga asilimia 10 ya mapato kwa vikundi vya vijana, wanawake na wenye ulemavu.

"Muongozo wa serikali katika asilimia hizo 10 ya mapato tuliyokusanya. tunatoa asilimia nne kwa vijana, nne zingine kwa wanawake na asilimia mbili kwa wenye ulemavu," alisema Hanifa.

Wakizungumza kwa niaba ya vijana wengine walioshiriki katika maonyesho hayo, Ibrahimu Kikoti na Sara Mosess, walisema kuwa kupitia mafunzo hayo, wameongeza maarifa ya kuwa wabunifu wa kuchangamkia fursa kwa kuzalisha bidhaa bora na kutafuta masoko ya uhakika.

Walisema kilichowafanya kuingia katika ujasiriamali ni kutokana na faida nyingi ikiwamo kuwa na uhuru wa kufanya kazi ambayo utaweza kuirithisha kizazi.

"Kilichonifanya mimi kuingia katika ujasiriamali ni mafanikio na maendeleo yanakuja pindi watu wanapochukua jukumu la kujiajiri inawasaidia kukuza kipato kwa kuwa kazi anayoifanya ni yake hivyo ataweza kuimudu kwa njia yoyote," aliongeza Sara.

Alisema vijana wengi wamekuwa wakilalamika kuwa ajira zimekuwa chache na hazipatikani kwa urahisi, suala hilo linatokana na wengi kutokujishughulisha na kazi na kuwa na ubunifu mdogo na kushindwa kutumia fursa.

Habari Kubwa