Vijana 45,000 kunufaika na mradi wa ujasiriamali

26May 2023
Ibrahim Joseph
DODOMA
Nipashe
Vijana 45,000 kunufaika na mradi wa ujasiriamali

NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amezindua mradi wa USAID Kijana Nahodha unaolenga kuwafikia vijana 45,000 watakaonufaika na masuala ya elimu ya uongozi, ujasiriamali, afya na ujuzi.

 

Akizungumza jana kwenye uzinduzi wa mradi huo unaotekelezwa na Shirika la T-MARC Tanzania kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Watu wa Marekani (USAID), Katambi alisema mradi huo ni muhimu katika kuwezesha maendeleo ya kiuchumi hasa katika kuwajengea vijana uwezo wa kutumia vizuri rasilimali zilizopo ili kuleta maendeleo katika jamii.

“Aidha, miradi ya aina hii ni uthibitisho wa ushirikiano thabiti na dhati uliopo baina ya Tanzania na Marekani, tunatambua mradi huu wa kijana nahodha utasaidia kufikia malengo tuliyokusudia ya kumkwamua kijana wa kitanzania azione fursa na kuwa na mchango kwa Taifa lake,”alisema.

Naibu Waziri Katambi aliwataka vijana wa mikoa ya Dar es salaam, Morogoro na mikoa yote ya Zanzibar kuchangamkia fursa ya mradi huo.

“Niwaombe pia viongozi na maofisa mliopo wa wizara zote zinazohusika na utekelezaji wa mradi huu kutoa ushirikiano ili kuhakikisha mradi huu unatekelezwa ipasavyo kwa kuzingatia sera na miongozo ya nchi iliyopo ili kuweza kuleta tija kwa maslahi mapana ya taifa letu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya vijana nchini,”alisema.

Naye, Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Kate Somvongsiri, alipongeza serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa jitihada za kuwainua vijana.

“Mradi huu utaleta manufaa kwa Tanzania na ni muhimu vijana wakatumia fursa ya mradi huu, nchi inayowekeza kwa vijana inapiga hatua kimaendeleo,”alisema.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la T-MARC Tanzania, Charles Singili, alisema mradi utainua vijana kufikia ndoto zao na unatekelezwa kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo ya nchi.

Mkurugenzi wa mradi huo, Dk.Tuhuma Tulli, alisema utatekelezwa kwa miaka minne (2022-2026) na unalenga kusaidia vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 25 hususan vijana ambao hawana elimu ya shuleni, wasio na ajira, wenye ulemavu, wasichana waliozaa katika umri mdogo na wenye maambukizi ya VVU.

Alisema mradi huo unafadhiliwa na USAID kwa Dola za Marekani Milioni 10.6 na utaenda kuboresha upatikanaji wa elimu ikiwa ni pamoja na elimu ya ufundi stadi, afya, uraia, ujasiriamali na uongozi