Vijana kunufaika mikopo ya mamilioni

14May 2017
Christina Mwakangale
Nipashe Jumapili
Vijana kunufaika mikopo ya mamilioni

VIJANA 2,500 wanaojiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), wahitimu wa elimu ya juu na wajasiriamali waliopo katika mpango wa kujiajiri, watapatiwa mkopo wa Sh. bilioni moja kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi  (NEEC) hilo, Beng’I Issa.

Aidha, vijana hao wanatakiwa kujiunga na vikundi vya kiuchumi hususan wanajishughulisha na usindikaji na kuongeza thamani mazao, ufugaji, uvuvi, usafirishaji, biashara, miradi inayotumia mali ghafi za ndani nchi zinazotengeneza ajira hasa kwa vijana.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi  (NEEC) hilo, Beng’I Issa, aliyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa utiliaji wa saini ya makubaliano kudhamini mikopo hiyo itakayotolewa na Taasisi ya Huduma Ndogo za Fedha  ya UTT Microfinance PLC, na kuwataka vijana kuonyesha nidhamu kwa kurejesha fedha hizo kwa wakati.

Alisema kiasi cha Sh. milioni 300 kimetengwa ili kudhamini mikopo itakayotolewa na taasisi hiyo itakayotolewa kwa riba ya asilimia 11.

“Walengwa wa mkopo huu ni vijana waliopata mafunzo ya ujasiriamali kupitia programu zinazoendeshwa na baraza za Kijana Jiajiri, vijana wanaojiunga na JKT na wahitimu vyuo vikuu,” alisema Issa.

Alieleza kuwa tatizo kubwa la ajira kwa vijana nchini linaweza kupunguzwa baada ya mafunzo ya ujasiriamali na kuwapatia mitaji kwa njia ya mikopo, inayotolewa na taasisi za kifedha kwa vijana.

Afisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, James Washima alisema hutengwa Sh. bilioni nane kila mwaka kwa ajili ya mikopo kwa Watanzania, wakiwamo vijana.

Alisema huduma ya mafunzo kuhusu uwekaji akiba, biashara na ujasiriamali kwenye matawi 12 Tanzania Bara na Zanzibar pia katika vituo 46 vinavyotoa huduma.