Vijana waaswa fedha

27Mar 2018
Said Hamdani
Lindi
Nipashe
Vijana waaswa fedha

MKUU wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga, amewataka vijana kujenga nidhamu na mipango mizuri katika kutafuta na matumizi ya fedha wanazozipata, ili ziwasaidie kuendesha maisha yao.

MKUU wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga.

Aidha, amesema wakitumia vizuri fedha hizo zitawasaidia kuanzisha na kukuza mitaji kwa walioamua kuanzisha miradi ya biashara.

Ndemanga aliitoa rai hiyo wakati akifungua mafunzo yaliyohusu kutambulisha programu ya ‘kijana jiajiri’ kwa vijana wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi.

Katika hotuba yake hiyo iliyosomwa na Kaimu Katibu Tawala Alice Kaluwa, Ndemanga alisema, ili vijana wafanikiwe kwenye maisha, ni wao kujenga nidhamu kwa fedha wanazozipata, na zile wanazokopa kutoka kwenye taasisi ikiwamo na Ilulu Saccos.

Ndemanga alisema ni vizuri vijana ambao ni tegemeo kubwa kwa nchi yoyote wakajitokeza kuchangamkia fursa zilizopo ndani ya maeneo yao zinazoletwa mbele yao, ikiwamo kujitokeza kuchukua mikopo ili iwasaidia kukuza mitaji kwa wale walioanzisha biashara.

“Vijana wangu katika kujiajiri kuna mambo muhimu mawili la kujali muda na matumizi mazuri ya fedha, mkiyaweza haya mmefanikiwa,” alisema Ndemanga.

Pia, aliwasisitiza washiriki hao wa mafunzo kuwa makini katika kupokea elimu wanayopewa kutoka kwa wawezeshaji, kwani itawajengea uwezo mkubwa wa kuendesha maisha yao na familia zao.

Mkuu huyo wa wilaya ya Lindi, aliwasisitiza vijana kutoogopa kuzitumia taasisi za fedha kuomba na kuchukua mikopo, ikiwamo ya asilimia 10 ya Mfuko wa Wanawake na Vijana zinazotengwa na halmashauri zao ambazo zinatokana na makusanyo yake ya ndani.

Awali akimkaribisha kufungua mafunzo hayo, Ofisa Mahusiano kutoka Mradi wa Ujenzi wa Gesi Asilia (LNG), Catherine Mbatia, alisema lengo la utoaji mafunzo hayo ni kuwawezesha vijana wapate elimu ya kuwajengea uwezo wa kujiajiri wenyewe badala ya kutegemea ajira ya serikalini.

Mbatia alisema mafunzo hayo yamefadhiliwa na kampuni tano zinazounda LNG kinachotarajiwa kujengwa mkoani Lindi wakati wowote, ni pamoja na Shell, StatOli, Ophir, Pavilion na Exxonmobil.

 

 

Habari Kubwa