Vijana wahimizwa kulima kibiashara wasisubiri ajira

30Oct 2016
Christina Mwakangale
aliyekuwa RUFIJI
Nipashe Jumapili
Vijana wahimizwa kulima kibiashara wasisubiri ajira

VIJANA wamehimizwa kujiingiza kwenye kilimo cha kisasa na cha kibiashara ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira.

Pia wametakiwa kujiunga katika vikundi vya kijasiriamali ili waweze kupata mikopo itakayowasaidia kununua mbegu na pembejeo.

Mkurugenzi wa Ushirika wa Wahitimu Wajasiriamali wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Sugeco), Revocatus Kimario, aliyasema hayo jana wilayani Rufiji, wakati akifunga mafunzo ya kilimo kwa vijana 44 kutoka maeneo mbalimbali walioshiriki mafunzo ya kilimo na ufugaji.

Alisema ipo haja ya Watanzania kuachana na kilimo cha mazoea na badala yake kukibadili na kuwa cha kibiashara ili kukuza uchumi na kuongeza fursa ya ajira kwa vijana.

Alibainisha kwamba vijana hao wamehitimu kwenye mradi wa mafunzo wa miezi ulioanza Agosti mwaka huu, ambao umelenga kufundisha wajasiriamali vijana 200 kwenye ufugaji na kilimo chenye tija kinachotumia teknolojia ya kisasa ili kuwekeza na kuanzisha miradi ya kuondoa umaskini na utegemezi wa kuajiriwa.

“Vijana waliokwishapatiwa mafunzo hadi sasa katika mradi huu ni 150, wametoka mikoa ya Kilimanjaro, Shinyanga, Singida, Iringa na Morogoro. Wanajifunza kwa vitendo namna ya kujiajiri katika kilimo,” alisema Kimario.

Aliongeza kuwa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) limetoa Dola za Kimarekani 98,646 sawa na zaidi ya Sh. Milioni 217 ili kufanikisha utekelezaji wa mradi.

Akifunga mafunzo hayo, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Fredrick Ngotoine, alisema halmashauri zinawajibika kuwapatia mikopo vijana ili kujiendeleza na kuanzisha shughuli mbalimbali ikiwamo kilimo cha kibiashara.

Alisema mkakati wa serikali katika kuimarisha uchumi kupitia viwanda, umetoa fursa ya ongezeko la uzalishaji wa mazao mbalimbali kama mboga , nafaka na matunda.

“Viwanda vinategemea zaidi malighafi kutoka mashambani, tukijikita katika kilimo na kuzalisha mazao, mbogamboga, matunda ya kutosha yatasindikwa na wakulima kujihakikishia mapato,” alisema Ngotoine.

Aliwaambia vijana hao wanahitaji kupatiwa mikopo na kwa mwaka huu wilaya ya Rufiji imetengewa Sh. milioni 165 kwa ajili ya vijana na wanawake.

Aidha kwa kipindi cha mwaka jana, jumla ya vikundi 10 kikiwamo chama cha kuweka na kukopa walipatiwa Sh. milioni 42 kwa ajili ya kuanzisha kilimo, ufugaji nyuki, kuku pamoja na sungura.