Vijana waonyeshwa fursa za kiuchumi

23Oct 2019
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Vijana waonyeshwa fursa za kiuchumi

VIJANA 212 wa Wilaya ya Chamwino wamehamasishwa kuchangamkia fursa zilizopo kwenye maeneo yao zikiwamo mikopo (fedha za mitaji), kilimo na ufugaji.

Wanachagizwa kuchangamka kutokana na mwitikio mdogo wa kuchangamkia fursa uliopo miongoni mwa vijana ikiwamo kuchukua mikopo inayotolewa na halmashauri.

Hayo yalielezwa jana na Mratibu wa Mradi wa kuwawezesha vijana kukamata fursa za kiuchumi wilayani humo, Emmanuel James, katika mafunzo ya ukamataji fursa.

Aliwaambia mradi huo unalenga kuwawezesha vijana kukamata fursa zilizopo kwenye maeneo yao na kuanzisha shughuli rafiki za kiuchumi ili kuboresha maisha yao.

"Pia kuwaunganisha vijana na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kupata masoko ya bidhaa zao, tunalenga vijana wa kike na kiume wenye umri kati ya miaka 18-35," alisema James.

Kadhalika, alisema mradi unatekelezwa katika kata nne za wilaya hiyo na Mtandao wa Mazingira Dodoma (DONET) kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Serikali la The Foundation for Civil Society(FCS).

James alisema mradi huo unagharimu Sh. milioni 40 na utatekelezwa hadi Februari 2020.

"Pamoja na vijana 212 kuhamasishwa pia tumewezesha uundwaji wa vikundi saba vya vijana kwenye vijiji hivyo ili kuchangamkia fursa ikiwamo mikopo inayotolewa na halmashauri wajikwamue kiuchumi," alisema James.

Aliongeza: "Tumewaunganisha vijana na wadau mbalimbali wa maendeleo kama taasisi za kifedha, kilimo, ufugaji na vyombo vya habari. Vijana waongeze ufahamu na ari ya kuthubutu kufanya kazi kwa namna yoyote yenye tija kwao," alisema.

Mratibu huyo alisema wamejipanga kuendesha elimu kwa njia ya vyombo vya habari kuhusiana na uwepo wa fursa za vijana zilizopo kwenye maeneo yao.

Aidha, watatoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanufaika wote wa mradi yatakayoendeshwa na Shirika la Viwanda Vidogo (Sido).

"Pia tutaunda majukwaa ya vijana ili kuongeza uhamasishaji wa vijana wengine, kuwawezesha vijana wajasiriamali kushiriki maonyesho ya wiki ya Azaki kitaifa kwa lengo la kuongeza maarifa, ubunifu na stadi katika shughuli zao za ujasiriamali," James alisema.

Habari Kubwa