Vijana watakiwa kukataa umaskini

15Mar 2019
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Vijana watakiwa kukataa umaskini

VIJANA wamekumbushwa kutokumbatia umaskini na badala yake wajitume kwa kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo kwa ajili ya kujiletea maendeleo.

Mtaalamu kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido), Michael Malembeka, alisema hayo jana wakati akitoa mafunzo ya kutengeneza na kusindika bidhaa mbalimbali za biashara kwa vijana.

Vijana hao kutoka majukwaa ya vijana Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam, wanajifunza kutengeneza sabuni za maji na miche na pia kusindika vyakula mbalimbali, matunda na kuoka mikate.

"Katika maisha kuna vitu viwili, utajiri na umaskini. Kijana unaweza kuamua kuzingatia mafunzo haya au kuyaacha na usitegemee mtu katika maisha yako, lakini ukumbuke umaskini una sifa kuu mbili," alisema Malembeka.

Alisema umaskini unaishi mahali ambapo unavumiliwa na kama hauwezi kuvumiliwa, utaondoka, na pia mkufunzi huyo alitaja sifa ya pili kuwa mtu asipoushughulikia, utamshughulikia.

"Hivyo msiuvumilie...utasikia mtu anasema mimi ni maskini nitafanyaje, hapa ina maana unauvumilia umaskini, vijana jitumeni kwa kupambana kwa dhati na adui huyu ili kuhakikisha mnafanikiwa katika maisha yenu," alisema.

Alisema mafunzo hayo ni njia mojawapo ya kupambana na umaskini iwapo watayazingatia, lakini vinginevyo wanaweza kutoka wakiwa hawana kitu cha kwenda kufanya katika maeneo yao.

Kwa upande wake mmoja wa viongozi wa taasisi inayoratibu mafunzo hayo,  Mpakani Tunaweza, Hussein Wamaywa aliwataka vijana kuhakikisha hawatoki watupu bali wawe na cha kujivunia.

"Mnafundishwa kutengeneza vitu vingi, na inawezekana kijana usipendelee kitu fulani, lakini ni muhimu upeleke ujuzi huo katika jukwaa lako, mwenzako anaweza kupenda ujuzi wa kile ambacho wewe hupendi," alisema Wamaywa.

Alisema vijana hao wakipeleka ujuzi huo katika majukwaa yao, inawezekana jukwaa likawa na wataalam wa kutengeneza bidhaa mbalimbali na hivyo mafunzo hayo kuleta tija.

"Hilo ndilo lengo la Mpakani la kuratibu mafunzo haya, cha msingi ni vijana kuwa makini kufuatilia kila hatua ambayo mkufunzi anaifanya ili wote mtakapotoka hapa muwe mmeiva kwa ujuzi za kutengeneza bidhaa kwa ajili ya maendeleo yenu," alisema.

Kiongozi huyo alisema muda wa siku tano kwa ajili ya mafunzo ya kutengeneza bidhaa, kusindika na kuoka unatosha kuwafanya vijana hao kupata kitu cha kujivunia kwa ajili ya maendeleo yao.

Habari Kubwa