Vijiji vyote kupata umeme Bunda

20Mar 2017
Ahmed Makongo
Nipashe
Vijiji vyote kupata umeme Bunda

SERIKALI imezindua mradi wa Umeme Vijijini (Rea) awamu ya tatu, ambao utaviwezesha vijiji vyote katika wilaya ya Bunda kupata umeme.

Mradhi huo ulizinduliwa juzi katika kijiji cha Mariwanda, wilayani Bunda na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani na kushuhudiwa na wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Akizungumza wakati akizindua mradi huo, Dk. Kalemani alisema utagharimu zaidi ya Sh. bilioni 41.15 na kwamba vijiji na vitongoji vyote vya mkoa wa Mara vitapata umeme, hali itakayoharakisha maendeleo ya wananchi.

Alimtaka mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha unakamilika kwa wakati uliopangwa wa miaka miwili.

"Hakuna kuruka kijiji hata kimoja, mkandarasi afanye kazi kwa saa 24 na awalipe kwa wakati vibarua atakaokuwa amewaajiri katika kazi hiyo."

Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha vijiji vyote nchini vinapata umeme ifikapo 2021.

Alisema pia umeme utasambazwa kwenye majengo yote ya taasisi na kwenye mitambo ya maji na kwamba mradi huo hauna itikadi za kisiasa hivyo kila kitongoji na vijiji vitapitiwa na kila mwananchi anastahili kupata huduma hiyo.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Gisima Nyamhanga, alisema kupitia Rea serikali imetekeleza mradi huo awamu ya kwanza na ya pili vizuri na sasa inaanza kutekeleza awamu ya tatu.

Habari Kubwa